Serikali imetumia kiasi cha shilingi  trilioni 10.69 kwa ajili ya ujenzi wa reli ya kisasa kwa kiwango cha kimataifa yenye urefu wa kilometa 1,219 kuanzia Dar es Saalam hadi Mwanza.

Hayo yamesemwa jana Bungeni na Waziri Mkuu Kassim Majalwa wakati akisoma bajeti ya Ofisi yake wa mwaka kwa mwaka 2024/2025, ambapo ameomba kuidhinishiwa na Bunge kiasi cha shilingi Bilioni 350,988.

Majaliwa alisema hadi  kufikia Februari 2024  ujenzi wa reli hiyo ulikuwa umefikia viwango vya kati ya asilimia 5.38 na asilimia 98.84.

“Tayari reli hiyo imeshaanza kufanyiwa majaribio kwa kipande cha Dar es Salaam hadi Morogoro.”alisema na kuongeza kuwa

“Kama nyote mlivyoshuhudia, majaribio ya treni hiyo ya mwendo kasi yalifanyika kwa mafanikio makubwa mwezi Februari, 2024, ni matarajio yetu kuwa huduma ya usafiri na usafirishaji itaanza ifikapo Julai, 2024 kwa kipande cha Dar es Salaam hadi Dodoma,”

Akifafanua kuhusu ujenzi wa reli hiyo, Waziri Mkuu amesema: “Ujenzi wa kipande cha Dar es Salaam – Morogoro (52.69, Makutupora – Tabora (Kilomita 371) umefikia asilimia 13.86, Tabora – Isaka (Kilomita 165) umefikia asilimia 5.38 na Tabora – Kigoma (Kilomita 506) umefikia asilimia 1.81 Kilomita 300) umefikia asilimia 98.84, Morogoro – Makutupora (Kilomita 422) umefikia asilimia  96.35.”

Kuhusu mradi wa kuzalisha umeme wa wa Julius Nyerere ambao unatarajiwa kuzalisha megawati 2,115, Waziri Mkuu Majaliwa alisema , utekelezaji wake umefikia asilimia 96.81 na kwamba kazi zote za mradi huo zinatarajiwa kukamilika mwishoni mwa Desemba, 2024. 

Aidha alisema  zoezi la kuwasha mtambo wa kuzalisha umeme lilifanyika na kufanikiwa kuingiza kwenye Gridi ya Taifa megawati 235 kutoka kwenye mtambo mmoja kati ya mitambo tisa itakayozalisha umeme katika mradi huo. 

Kuhusu uboreshaji wa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), Waziri Mkuu alisema Serikali imekamilisha malipo ya sh. bilioni 753 kwa ajili ya ndege tatu aina ya Boeing 737-9 Max (ndege mbili) na Boeing 787-8 (ndege moja).

 “Ndege mbili aina ya Boeing 737-9 Max ziliwasili nchini Oktoba, 2023 na Machi, 2024 na nyingine moja inategemewa kuwasili Aprili, 2024 na hivyo kulifanya Shirika hilo liwe na jumla ya ndege 16.”alisema

Kuhusu mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta ghafi la Afrika Mashariki kutoka Hoima, Uganda hadi Chongoleani, Tanga lenye urefu wa km. 1,443, Waziri Mkuu alisema Serikali tayari imechangia jumla ya dola za Marekani milioni 268.77 sawa na asilimia 87.27 ya hisa zake.

“Hadi kufikia Machi, 2024 baadhi ya shughuli zilizofanyika ni kukamilisha ulipaji wa sh. bilioni 34.93 zikiwa ni fidia  kwa wananchi 9,823 kati ya 9,904 wanaopisha eneo la mradi; kukamilika na kuzinduliwa kwa kiwanda cha kusimika mifumo ya kupasha joto na kuzuia upotevu wa joto kwenye bomba kilichopo Wilaya ya Nzega; na kuanza ujenzi wa matanki manne yenye ujazo wa mapipa 500,000 kila moja ya kuhifadhia mafuta ghafi kabla ya kupakiwa kwenye meli katika eneo la Chongoleani, Tanga.”alisistiza

Kuhusu mradi wa kiwanda cha sukari Mkulazi, Waziri Mkuu amesema ujenzi wake umefikia asilimia 99 na umegharimu sh. bilioni 320.05 na umetoa fursa za ajira 1,996.

 “Kiwanda hicho kimeanza uzalishaji tangu Desemba, 2023 na hadi kufikia Machi 2024, tani 1,851 za sukari zimezalishwa na kupelekwa sokoni. Matarajio ya kiwanda ni kuzalisha tani 50,000 kwa mwaka ifikapo mwaka 2026/2027,”

Kuhusu mradi wa daraja la Kigongo – Busisi (Mwanza) lenye urefu wa kilomita 3.2 pamoja na barabara unganishi yenye urefu wa kilomita 1.66 kwa kiwango cha lami, Waziri Mkuu amesema ujenzi wake umefikia asilimia 84.47 na unatarajiwa kukamilika Desemba, mwaka huu. Mradi huu utagharimu sh. bilioni 716.33.

Mradi mwingine ambao Waziri Mkuu ameuelezea ni kiwanja cha ndege cha kimataifa cha Msalato kilichopo Dodoma ambacho ujenzi wake umefikia asilimia 54.1 na kwamba hadi kufikia Februari, 2024 zimetumika sh. bilioni 107.64. 

Amezitaja kazi zinazoendelea kuwa ni ujenzi wa barabara ya kuruka na kutua ndege, barabara ya viungio, maegesho ya ndege pamoja na usimikaji wa taa za usalama na kuongozea ndege. Ujenzi wa jengo la abiria na majengo mengine utekelezaji umefikia asilimia 17.1.

Kuhusu ujenzi wa meli ya MV. Mwanza “Hapa Kazi Tu”, Waziri Mkuu amesema umefikia asilimia 93 ambapo Serikali imetumia dola za Marekani milioni 44.823 sawa na asilimia 90.87 ya gharama zote za mradi huu ambao unatarajiwa kukamilika Mei, 2024. “Kukamilika kwa mradi huu kutaboresha huduma za usafiri wa abiria na mizigo kwa njia ya meli katika mikoa ya Kanda ya Ziwa na nchi za jirani za Kenya na Uganda, na kufungua nchi kiuchumi pamoja na kuchochea ukuaji wa sekta ya utalii,” alisema waziri Mkuu Majaliwa 

By Jamhuri