Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia, Songwe

Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe linamshikilia Yusta Mwanyonga (27) Mkazi wa Kijiji cha Senjele, wilayani Mbozi kwa kosa la wizi wa mtoto mchanga wa miezi miwili.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Alex Mkama, amesema mtuhumiwa huyo aliiba mtoto huyo Oktoba 3, mwaka huu, katika kijiji hicho kilichopo kata ya Nanyala Wuilayani Mbozi.

Amesema mtuhumiwa huyo alifika nyumbani kwa mama mwenye mtoto aliyemtaja kwa jina la Sarah Sirini mkazi wa kijiji cha Senjele majira ya saa 7:00 mchana na kuomba ambebe mtoto huyo na kwenda naye matembezi.

Mkama amesema mtuhumiwa alipewa mtoto kwa kuwa mama wa mtoto alimuamini kwa sababu ni mtu aliyekuwa akifahamika kijijini hapo.

Amesema baada ya mtuhumiwa huyo kupatiwa mtoto hakuweza kumrejesha mapema hadi majira ya jioni hali ambayo ilimshtua mama mwenye mtoto hivyo walitoa taarifa kwa ndugu jamaa na kuanza kumtafuta.

“Baada ya jitihada za kumtafuta mtoto kuendelea kwa muda kutoka kwa familia, ndugu,jamaa na marafiki,mtoto huyo alipatikana majira ya jioni akiwa ametelekezwa kwenye shamba la kanisa kijijini hapo” amesema.

Amesema mtoto huyo alipatikana majira ya saa 12:00 jioni akiwa ametupwa kwenye shamba la kanisa baada ya wananchi kusikia kilio.

Kamanda Mkama amesema mtuhumiwa huyo alikamatwa akiwa amekimbilia katika mji wa Mbalizi katika Wilaya ya Mbeya vijijini, Mkoani Mbeya.

“Tunaendelea kufanya uchunguzi ili kujua lengo la mtuhumiwa la kuiba mtoto lilikuwa ni lipi na baada ya hapo atafikishwa mahakamani’alifafanua Mkama

Please follow and like us:
Pin Share