Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limewakamata, linawashikilia na kuwahoji kwa kina watuhumiwa watano (5) kwa tuhuma za kutenda makosa mbalimbali ya kimtandao.

Akizungumza na Waandishi wa habari leo Machi 14, 2024 jijini Dar es Salaam, Kamanda Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro amesema wamekamatwa kutokana na ufuatiliaji maalum unaoendelea unaofanywa na Jeshi la Polisi kwa kushirikiana kikosi kazi maalum cha kuzuia na kupambana na makosa ya kimtandao.

Amewataja waliokamatwa ni pamoja na
Obadia Kwitega (35) mkazi wa Kigamboni na Issa Mwamba (28) mkazi wa Tabata Segerea.

“Wamekamatwa kwa tuhuma za kumiliki
televisheni ya mtandaoni ya kwenye Youtube iliyotambulika kwa jina la Jamii
Digital, na akauti ya mtandao wa X iitwayo SUKUNUNU 01, waliyokuwa wanazitumia kusambaza taarifa za uongo na za uchochezi kuhusu viongozi wakuu wa Serikali.

“Baadhi ya taarifa zao zilisomeka “MKAKATI WA SIRI JANUARY MAKAMBA KUMNG’OA RAIS SAMIA 2025” amesema Kamanda Muliro.

Katika hatua nyingine Jeshi hilo limemkamata pia Frank Mbetu (35) mkazi wa Ligula, Mtwara kwa tuhuma za kujifanya mtumishi wa Serikali ngazi ya Katibu Mkuu Kiongozi na kujipatia pesa kwa njia ya udanganyifu kuwa angewapa watu kazi serikalini au kupandishwa vyeo.

Amekamatwa pia Honest Mgona (47) mkazi wa Mabwepande kwa kujipatia pesa kwa njia ya udanganyifu kuwa ametumwa na Mohamed Nchengerwa (MB), Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na serikali za mitaa kusambaza mitungi gesi kwa wananchi na baadae kuwatapeli kwa kuwadai pesa za usafiri.

“Mwingine ni Edwin Kasebele@ Marlin (24) Mkazi wa Mapelele, Mbeya
anayetuhumiwa kusambaza taarifa za uongo kupitia mtandao wa kijamii wa ‘Facebook’ na ‘Whatsapp’ kuwa anafanya biashara ya vitenge na hivyo kujipatia pesa kwa udanganyifu kutoka kwa watu mbalimbali,” amesema.

Amefafanua kuwa watuhumiwa hao wamekutwa wakiwa na simu 7 na kadi za za simu 13 za kampuni mbalimbali ambazo wamekuwa wakitumia kama nyenzo kutekeleza uhalifu wao.

“Kutokana na vitendo hivi vya kihalifu kwa njia ya mtandao, Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linatoa rai kwa wananchi kuwa makini na matumizi ya mitandao na Jeshi la Polisi linaendelea kuwachukulia hatua kali watu wengine wanaokiuka sheria, kanuni na taratibu za matumizi sahihi ya mitandao.

“Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linawahimiza wananchi kuendelea kutoa taarifa kwenye kituo cha Polisi kilicho karibu ili hatua stahiki zichukuliwe haraka. Pia linawahimiza wananchi kuendelea kutotoa CV, namba ya NIDA au vitambulisho, nywila (password) au namba ya siri (PIN) kwa mtu yeyote bila kuwa na uhakika na kinachofanyika,” amesema Muliro.

By Jamhuri