Na Allan Kitwe, JamhuriMedia, Tabora
Watu 4 wamekamatwa na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) Kanda ya Magharibi na kupandishwa kizimbani kwa tuhuma za kukutwa na vibunda 546 sawa na kilo 166.71 za dawa za kulevya aina ya mirungi.
Watuhumiwa hao wamekamatwa April 17, mwaka huu, wilayani Igunga, mkoani Tabora na kufikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Igunga na kufunguliwa kesi ya uhujumu uchumi namba 4764 ya mwaka 2026.
Waliokamatwa na kufikishwa katika Mahakama hiyo ni wanawake 3 na mwanaume 1, ambao majina yao ni Maige Kasawa (36), Nyanzala Marwa (25), Manungwa Makoye (38) na Hamisa Hussein (50), wote ni wakazi wa Igunga.
Wakiwa Mahakama hapo, Mawakili wa Jamhuri walimwomba Hakimu apokee dawa hizo kama kielelezo cha ushahidi na atoe amri ya kuteketezwa kwa kuwa kina madhara kwa mtunzaji na kinaharibika kila muda unavyozidi kwenda.
Mahakama chini ya kifungu cha 38 kifungu kidogo cha 2, 3, 4 na 5 cha sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya sura ya 95 marejeo ya mwaka 2023 iliridhia kutekelezwa dawa hizo, baada ya washtakiwa kutokuwa na pingamizi.
Baada ya kutolewa idhini, zoezi la uteketezaji dawa hizo lilitekelezwa mara moja huku likihusisha washtakiwa wenyewe na kushuhudiwa na Mkuu wa Wilaya hiyo Bi. Sauda Mtondoo.
Kamishna wa DCEA Kanda ya Magharibi, Christina Rweshabura alibainisha kuwa wamejipanga vizuri na wanamikakati endelevu na ya dhati ya kuendelea Kudhibiti na Kupambana usafirishaji, uuaji pamoja na matumizi ya dawa hizo.
Hata hivyo ilielezwa mahakamani hapo kuwa uchunguzi wa tuhuma hizo bado unaendelea na kesi itatajwa tena tarehe 6 Juni mwaka huu huku watuhumiwa wakirudishwa mahabusu kwa kesi yao kukosa mdhamana.

