Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia,Dodoma

Katika kipindi cha utekelezaji wa miaka 60 ya Muungano, Tanzania imefanikiwa kutoa viongozi mahiri kuongoza taasisi za kikanda na kimataifa ikiwa ni ishara ya kuaminiwa na mataifa mengine.

Baadhi ya nafasi ambazo Tanzania imeongoza ni uteuzi wa Mheshimjiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kama Mwenyekiti Mwenza wa Mkutano wa Kilele wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia Barani Afrika utakaofanyika Paris, Ufaransa mwezi Mei 2024.

Naibu Waziri wa Mambo ya nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk amebainisha hayo leo Aprili 18,2024 Jijini hapa kwenye mkutano wake na vyombo vya habari kuhusu mafanikio ya miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Amesema,Tanzania pia ilitoa Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ambapo Dkt. Salim Ahmed Salim aliongoza Vikao Vinne vya Baraza hilo mwaka 1979 na 1980 ikiwa ni pamoja na Dkt. Salim Ahmed Salim ambaye alihudumu kama Katibu Mkuu wa Umoja wa Afrika (OAU).

Amewataja Watanzania wengine kuwa ni pamoja na Dkt. Asha-Rose Migiro kuwa Naibu Katibu Mkuu wa kwanza kutoka Afrika,Balozi Getrude Mongela kuwa Rais wa Bunge la Afrika, Dkt. Stergomena Tax kuwa katibu Mtendaji wa SADC, Balozi Juma Mwapachu katibu Mkuu wa EAC; Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb.) na Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu (ICGLR); Profesa Anna Tibaijuka kuwa Naibu Katibu Mkuu na Mkuu wa Shirika la Maendeleo ya Makazi la Umoja wa Mataifa (UN-HABITAT) .

Wengine ni Mkuu wa Ofisi za Umoja wa Mataifa Nairobi (UNON), Bi. Joyce Msuya, Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) na hivi karibuni Spika wa Bunge la Tanzania Mhe. Dkt. Tulia Ackson (Mb.) kuchaguliwa kuwa Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) huku akimtaja Dkt. Tulia kuwa ni mwanamke wa kwanza kutoka barani Afrika kushika wadhifa huo.

Kuhusu mwenendo wa uwakilishi ameeleza kuwa uhusiano kati ya Tanzania na nchi mbalimbali umeendelea kuimarika ambapo Tanzania imefungua Balozi na Ofisi za Uwakilishi katika nchi mbalimbali za kimkakati ikiwa ni sehemu ya kuimarisha utekelezaji wa Sera ya Mambo ya Nje hususan Diplomasia ya Uchumi.

“Serikali ya Awamu ya Sita imefungua Balozi mpya mbili za Vienna, Austria na Jakata, Indonesia na Konseli Kuu mbili za Lugumbashi na Guangzhou, China’Ufunguzi wa Balozi hizo umeifanya Tanzania kufikisha jumla ya Balozi na Ofisi za Uwakilishi zipatazo 45 na Konseli Kuu tano,Kadhalika Tanzania ni mwenyeji wa nchi na mashirika ya kimataifa zaidi ya 90 ikiwemo Konseli Kuu ambazo baadhi yake zipo Zanzibar kama vile China, Oman, India na Umoja wa Falme za Kiarabu, “amesema.

Ameeleza kuwa uwepo wa Konseli kuu umechangia kuimarika kwa ushirikiano wa uwili, ujirani mwema na kuongezeka kwa manufaa katika sekta za ushirikiano ikiwemo biashara, utalii, uwekezaji, uchumi wa buluu na kubidhahisha kiswahili.

Ameeleza mafanikio mengine kuwa ni Tanzania imefanikiwa kuwa mwenyeji wa Taasisi za Kimataifa kama ishara mojawapo ya kuaminika na kukubalika na nchi nyingine.

“Miongoni mwa taasisi na mashirika ya kimataifa yenye makao makuu hapa nchini ni pamoja na Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki; Mahakama ya Afrika Mashariki; Bunge la Afrika Mashariki; Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu na Kamisheni ya Kiswahili ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, “amesema na kuongeza ;

Mafanikio mengine ni Bodi ya Ushauri ya Masuala ya Rushwa ya Umoja wa Afrika; Taasisi za Umoja wa Mataifa, Taasisi ya Afrika ya Sheria za Kimataifa; Chuo cha Upasuaji cha Afrika Mashariki, Kati na Kusini; Umoja wa Posta Afrika; Mahakama ya Kimataifa ya Masalia ya Kesi za Mauaji ya Kimbari ya Rwanda na Kituo cha SADC cha Kupambana na Ugaidi. Uwepo wa taasisi hizi una manufaa ya kiuchumi, kijamii, kisiasa, “amesema