Mil. 622/- kulipa fidia Njombe kwa kaya 31

Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa, amemuagiza Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi kutenga kiasi cha Sh.  milioni  622 kwa ajili ya kulipa fidia kwa kaya 31 za wananchi waliopisha ujenzi wa barabara ya Ndulamo-Nkenja-Kitulo Km 42.2 inayojengwa kwa kiwango cha lami.

Ameeleza kuwa katika ujenzi wa barabara hiyo inayounganisha Mkoa wa Njombe na Mbeya, kilometa 7 tayari zimekamilika kujengwa kwa kiwango cha lami  na kusisitiza kuwa ujenzi wake utakapokamilika utaleta mapinduzi makubwa ya kiuchumi.

“Namuelekeza Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, tuweke kipaumbele kikubwa ili hizi sh milioni 622 zije wananchi ambao wapo kwenye hiki kipande cha barabara ya Njombe Mjini hadi makete waweze kulipwa fidia ambayo wameisubili kwa muda mrefu,” amesema Bashungwa

Bashungwa ametoa agizo hilo wakati akiongea wananchi wa Ujuni wilaya Makete mkoani Njombe katika ziara ya kukagua utekelezaji wa miundombinu ya barabara iliyokamilika na inayoendelea kujengwa kwa kiwango cha lami.

Aidha, Bashungwa amemuagiza Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) mkoa wa Njombe Ruth Shaluwa, kuweka  kilometa 2 kila mwaka katika mpango kuhusu ujenzi wa barabara hiyo ili iweze kukamilika kwa haraka.

Naye, Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Anthony Mtaka, ameelezea umuhimu wa barabara hiyo  katika Wilaya ya Makete kuwa ndiyo inayoongoza kwa ukusanyaji wa mapato kutokana na uzalishaji mkubwa wa viazi mviringo ambapo Sh milioni 700 inakusanywa kwa mwaka.

Kwa upande wake Mbunge wa Makete, Festo Sanga, ameiomba Serikali kuikamilisha barabara hiyo inayounganisha mkoa huo na mkoa wa Mbeya kwani ni ya kimkakati na kiuchumi kutokana na uwepo wa Hifadhi ya Kitulo, uzalishaji wa mazao, miti na maziwa.