Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa leo Jumanne Januari 23, 2024 amekutana na kufanya mazungumzo na Naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Watu wa China, Liu Guozhong ambaye aliwasili nchini jana Jumatatu Januari 22, 2024 kwa ziara ya kikazi ya siku tatu.

Mazungumzo ya viongozi hao wawili yamefanyika Ofisi Ndogo ya Waziri Mkuu, Magogoni jijini Dar es Salaam kuhudhuriwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko na viongozi wa Serikali kutoka Jamhuri ya Watu wa China na Tanzania.

Waziri Mkuu ujio wa kiongozi huyo unatokana na mahusiano mazuri yaliyopo tangu enzi za Waasisi wa nchi hizo mbili ambapo mahusiano hayo yameendelea kunufaisha wananchi wa Tanzania na China, kiuchumi, kiutamaduni na kisiasa.

“Mazungumzo yetu leo yamegusa masuala ya kiuchumi tukizingatia propramu ya sasa ya nchi ya Tanzania ya kukuza uchumi, pia tumezungumzia masuala ya biashara na uwekezaji ikiwemo ujenzi wa miundombinu kama vile viwanja vya ndege, barabara na uboreshaji wa nishati ya umeme.”

Kuhusu uwekezaji amesema kuwa, China inafanya uwekezaji hapa nchini ikiwemo kwenye ujenzi wa miundombinu akitolea mfano ujenzi wa reli ya kati ambao sasa unaendelea na China imetoa mkopo wa gharama nafuu, pia imewekeza kwenye mradi wa Makaa ya Mawe Liganga na Mchuchuma na Viwanda.

Katika hatua nyingine, Majaliwa amesema kuwa, viongozi hao wamezungumza kuhusu uimarishaji wa mipango mikakati ya nchi ya China kwa nchi za Afrika (FOCAC) ambapo FOCAC imedhamiria kusimamia maendeleo ya Afrika katika afya, elimu, miundombinu na nishati na kwamba Tanzania tayari imewasilisha miradi nane.


Ameongeza kuwa, Tanzania imeieleza China kuhusu nia yake ya kuukuza uchumi wa buluu kwani kuna fursa za kutosha na uwekezaji bado unahitajika hivyo imealika kampuni kubwa kutoka China kuwekeza kwenye eneo hilo kufanya uvuvi wa kisasa hivyo Tanzania iwe wazalishaji wakuu wa samaki.

Amesema kuwa, viongozi hao wamezungumzia Sekta ya Afya wakigusia maboresho ya Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) ili iweze kutoa huduma bora zaidi ambapo Serikali ya China imefadhili suala hilo na ushirikiano wa madaktari pamoja na mafunzo ya Watanzania nchini China.

Pia, wamezunguzia kuhusu uboreshwaji wa sekta ya kilimo na Naibu Waziri Mkuu wa China ameahidi kuwakutanisha Mawaziri wa Kilimo wa nchi hizo wajadiliane na waone maeneo ya ushirikiano na teknolojia inayohitajika kuboresha sekta hiyo hasa kwenye eneo la umwagiliaji ambapo kunahitajika mitambo mikubwa kuboresha suala la umwagiliaji.

Amesema China imekubali Soko la nchi hiyo litumike kama soko la bidhaa za Tanzania na wametamka kuwa wana mahitaji kubwa ya nafaka kama vile maharage ya soya, korosho na mazao mengine, hivyo amewasihi Watanzania wachangamkie fursa hizo.

Amesema Tanzania itaendelea kuimarisha ushirikiano wake na China ili kuweza kufanya biashara, kushirikiana katika siasa na masuala ya kijamii kwa ujumla wake.

Kwa upande wake, Mhe. Liu amesema China itaendelea kuifanya Tanzania nchi ya kimkakati katika mashirikiano kwenye sekta za Biashara, uwekezaji na kilimo ikiwemo kuwa soko la mazao ya Parachichi, Maharage pamoja na Korosho.