Dar es Salaam

Na Christopher Msekena

Mamia kwa maelfu ya wasanii wa muziki nchini wameufungua mwaka 2022 kwa kicheko wakipokea gawio (au mirabaha) ya kazi zao kutoka serikalini kupitia Chama cha Hakimiliki (COSOTA).

Katika hafla iliyofanyika hivi karibuni jijini Dar es Salaam, wasanii kadhaa walipewa mfano wa hundi ya malipo ya fedha za mirabaha iliyotokana na makusanyo kwenye maeneo mbalimbali yanayotumia muziki.

Hatua hiyo kwenye tasnia ya muziki imefikiwa baada ya agizo la Rais Samia Suluhu Hassan alilolitoa mwaka jana kwa COSOTA kuhakikisha wasanii wanalipwa mirabaha yote iliyotokana na nyimbo zao kutumika kwenye nyumba za starehe, vyombo vya usafiri, vyombo vya habari na maeneo mengine.

Kwa muktadha huo maelfu ya wasanii wakajikuta kwenye orodha ya malipo ya mirabaha ambayo imegusa aina mbalimbali za muziki kama Bongo Fleva, Injili, Kwaya, Dansi, Bendi, Taarabu, muziki wa asili na nyinginezo.

Katika awamu hii ya kwanza ya mirabaha iliyoanza kutolewa wiki mbili zilizopita, mpaka sasa imekuwa ikizua gumzo kwa mambo mbalimbali yaliyoambatana na gawio hilo.

Mosi, ni ushiriki wa wanamuziki pekee kwenye mirabaha bila kuwahusisha watayarishaji ambao ni kiungo muhimu katika muziki wowote. 

Gawio linapokwenda kwa msanii bila mtayarishaji kuwamo linatengeneza taswira mbaya licha ya lengo zuri la COSOTA chini ya serikali, hivyo ni muhimu hilo likazingatiwa ili kuweka usawa na kila aliyeshiriki kuandaa muziki apate chake.

Prodyuza S2kizzy ni miongoni mwa watayarishaji wakubwa ambao waliliona hilo mapema na kuiomba serikali kuwaangalia pia wanaoandaa muziki kwa sababu hakuna muziki bila maprodyuza ambao wanafanya kazi kubwa.

Hivyo basi licha ya kazi kubwa kufanywa na Wizara ya Sanaa na COSOTA kuna umuhimu wa kuongeza wigo wa walengwa wa mirabaha ili isiishie kwa wasanii tu, iende mpaka kwa watayarishaji wa muziki.

Mbali ya watayarishaji kutoorodheshwa kwenye awamu hii, kuna kundi jingine la wasanii ambao nao wamekuwa wakitamani kujua hatima yao.

Ukiangalia orodha iliyotolewa utagundua ni wasanii wa muziki pekee ndio wametajwa lakini sanaa ina wigo mpana, sanaa si muziki au filamu peke yake.

Ni bahati kuwa muziki ni kitu ambacho kipo kwenye maisha ya kila mtu kila siku na kinatumika mara kwa mara kuliko sanaa nyingine lakini hiyo haiondoi umuhimu wa sanaa hizo.

Wasanii wa filamu, wachoraji, wafinyanzi, wachongaji na sanaa nyingine wanahitaji kuona na wao wakinufaika na mirabaha kama ambavyo wanamuziki wananufaika.

Kwa hiyo ingependeza kuona kadiri kazi za wasanii wa sanaa nyingine zikitumika hivyo hivyo na wao wapate gawio kama ilivyofanyika kwenye muziki.

COSOTA wamefanya kazi nzuri ya kupongezwa na inaingia kwenye historia ya sanaa nchini kwamba mwaka 2022, wasanii wameanza kupokea mirabaha yao kwa uwazi kwa msisitizo wa Rais Samia.

Licha ya kazi hiyo njema na nzuri, COSOTA sasa wanapaswa kuingia kazini upya na kutengeneza njia nyingine nzuri za wasanii wote kunufaika na si wa muziki pekee.

Natambua ndiyo kwanza tumeingia kwenye mfumo huu wa kukusanya na kuwagawia wasanii mirabaha yao, si jambo baya tukijifunza kwa mataifa yaliyoendelea ambayo wasanii wote hunufaika.

Kuna mataifa yaliyotutangulia kwenye masuala ya teknolojia ya ukusanyaji wa mirabaha na wasanii wake wanapokea pesa nyingi pia nchi zao zinajipatia kipato kupitia kodi kwa wasanii hao.

Ndiyo maana wasanii wake wanaweza kuishi vizuri hata wasipotoa kazi mpya, kazi zile zile za zamani zinawanufaisha wao na hata baada ya wao kufariki dunia vizazi vyao pia hunufaika.

Usishangae kuona majarida makubwa kama Forbes, yanatoka na orodha ya wasanii walioingiza fedha nyingi wakiwa wamekufa, hiyo yote ni kazi ya vyama vyao vya Hakimiliki kukusanya vizuri mirabaha na kuhakikisha wasanii wote wanapata.

Natamani siku moja hiyo iwepo Tanzania ili familia za wasanii waliotangulia mbele za haki zisiwe ombaomba, ziwe na uhakika kwa kupata mirabaha ya wapendwa wao.

Naamini COSOTA wanaweza kutufikisha huko kwa sababu tayari wametuonyesha mwanzo mzuri hivyo baada ya miaka kadhaa watakua kiteknolojia na kugusa wasanii wa sanaa zote.

Mchakato huu unatia motisha wa kufanya kazi nzuri zaidi za kibunifu kwa wasanii wachanga na ambao kwa bahati mbaya hawajapata fedha nyingi ili katika awamu zijazo za mirabaha waweze kuondoka na mzigo wa maana kama walivyofanya kina Kwaya ya Mtakatifu Cecilia Arusha Alikiba, Rose Muhando, AY, Ibraah, Harmonize, Diamond Platnumz na Mwana Fa.

Wasanii wengine waliofanya vizuri kwenye awamu hii ya mirabaha ni  Ray C, Lady Jaydee, Abby Chamz, Luludiva, Mwasiti, Linah Sanga, Anjella, Maua Sama, Saraphina, Nandy, Mabantu, Jay Melody, Juma Jux, Darassa na Profesa J.

By Jamhuri