Februari 4, mwaka huu, Rais Samia Suluhu Hassan, ametengua uteuzi wa wakurugenzi watendaji wa halmashauri za wilaya za Buchosa, Iringa, Mbeya na Singida Mjini kwa matumizi mabaya ya fedha za miradi ya maendeleo na upotevu wa mapato katika halmashauri hizo.

Rais Samia ametangaza uamuzi huo akiwa njiani Magu kuelekea Musoma mkoani Mara yalipofanyika maadhimisho ya miaka 45 tangu kuanzishwa kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Siku akitangaza matumizi ya fedha za mkopo wa masharti nafuu kutoka Shirika la Fedha Duniani (IMF), Rais Samia, amesema kama mkurugenzi anataka kuona rangi yake halisi azichezee. 

Pia Rais Samia akaagiza uchunguzi uendelee kwa yule wa Geita na timu yake inafanya uchunguzi na wakimletea makosa kama hayo naye atatenguliwa.

Kimsingi, sisi Gazeti la JAMHURI tunapongeza hatua ya ma-DED hao kutenguliwa katika nafasi zao lakini tunadhani isiishie hapo, bali wanapaswa kufikishwa mahakamani.

Kwa sababu kwa muda mrefu sasa baadhi yao katika maeneo mengi hapa nchini wanatuhumiwa kufanya makosa ya kutafuna au kuchepusha fedha za miradi ya maendeleo na hiyo ni kwa mujibu wa ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Mathalani, baadhi wamekuwa wakihusika kuingiza watu wasiokuwa na sifa katika mpango wa kunusuru kaya maskini unaosimamiwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf), kutofikisha ruzuku stahiki kwa walengwa huku baadhi ya viongozi wa kamati za mpango huo kuwa ni miongoni mwa walengwa na wengine kuchukua malipo ya waliofariki dunia au kuhama maeneo yao.

Pia tunawaomba katika maeneo mengine kuanza kutumia vizuri fedha zinazotolewa kwa ajili ya miradi ya maendeleo ya wananchi na wote watakaobainika kutumia fedha hizo vibaya washughulikiwe kwa mujibu wa sheria.

Mbali na hayo, pia tunaiomba serikali kuanza kuyafanyia kazi mapendekezo ya CAG ya hatua mbalimbali za kuwachukulia si ma-DED hao peke yao, bali na watendaji wengine katika halmashauri mbalimbali ambao ni ‘mchwa’ wanaoongoza kutafuna fedha za miradi ya umma.

Kwa sababu wao ndio vinara wa kukwamisha maendeleo ya miradi mbalimbali katika maeneo tofauti na kusababisha adha kwa wananchi.

Pamoja na mambo mengine, tunaiomba serikali isiwape nafasi ya kuwalea watendaji wanaoweka masilahi yao mbele badala ya kuangalia wananchi katika kutekeleza miradi hiyo, kitu kinachosababisha mingi kutekelezwa chini ya kiwango bila kuzingatia thamani ya fedha, huku baadhi ya watendaji katika halmashauri walifikia hatua ya kuandaa maandiko ya kuomba fedha za ufadhili wa miradi ya maendeleo ya wananchi lakini zikipatikana wanagawana na kuzitumia kwa shughuli zao binafsi badala ya kuzingatia malengo yake kama ilivyokusudiwa.

By Jamhuri