Mji wa Kherson ulioko karibu na eneo la mapambano kusini mwa Ukraine, umetangaza amri ya kutotoka nje kwa saa 58 kuanzia Ijumaa jioni.

Hayo yameelezwa leo na mkuu wa utawala wa kijeshi wa Kherson, Oleksandr Prokudin, wakati ambapo vikosi vya Ukraine vikijiandaa na mashambulizi ya kupambana na vikosi vya Urusi majira ya machipuko.

Katika mtandao wa Telegram, Produkin amesema katika muda huo, ni marufuku watu kutembea kwenye mji huo. Aidha, raia watatu wameuawa katika shambulizi la Urusi lililotokea leo kwenye soko kubwa katika mji wa Kherson.

Wakati huo huo, Idara ya Usalama ya Shirikisho la Urusi, FSB, imesema kuwa watu saba wanaohusishwa na shirika la kijasusi la Ukraine wamekamatwa katika jimbo la Crimea.

FSB imesema mashambulizi dhidi ya Sergei Aksyonov gavana wa jimbo hilo linaloungwa mkono na Urusi, pamoja na maafisa wengine, yamezimwa.

By Jamhuri