Mwandishi Wetu

Shahidi wa nne katika kesi ya kujeruhi
inayomkabili mfanyakazi wa benki ya CRDB, Ibrahim Masahi, Careen Wiliam ameieleza mahakama kuwa mume wake Deogratus Minja wakati wanampeleka Hospitali ya Bochi aliwaeleza kuwa amejeruhiwa na jirani yake Masahi.

Careen amedai hayo leo mbele ya Hakimu Mkazi, Amos Rweikiza wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni, Dar es Salaam wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kusikilizwa kwa mashahidi wa upande wa mashitaka.

Akiongozwa na Wakili wa Serikali, Salma Jafari, Careen amedai kuwa yeye anaishi Mbezi Msakuzi na mume wake pamoja na watoto, Februari 11, 2023 majira ya saa 2:00 usiku alikuwa nyumbani kwake, jirani yake Mama Imma alimpigia simu kwa kumtaka afike nyumbani.

“Alinitaka nifike nyumbani kwake kuna tatizo limetokea, lalini hakunieleza kwenye simu tukio hilo, nilipofika nilikuta mume wangu akiwa amelala chini akiomba msaada huku akiwa na majeraha mwilini mwake na damu zikiwa zinamtoka,”

” Niliwajulisha ndugu zake kabla sijampeleka hospitali nikiwa na majirani zangu Lucas, Aidan, Ishengoma na Kume,
tulimchukua na kumpeleka Hospitali ya Bochi ili kuweza kuokoa afya, tukiwa njiani tunampeleka hospitali alitueleza kwamba amejeruhiwa na jirani yetu aitwaye Ibrahim Masahi wakati akitoka kazini,”amedai Careen

Hata hivyo, amedai kuwa baada ya kumpeleka mume wake hospitalini hapo alipata matibabu, na kisha kupewa rufaa ya kwenda Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa matibabu zaidi.

Wakati akiendelea kutoa ushahidi wake , Wakili Jafari alimtaka shashidi huyo kumtambua mshitakiwa (Masahi) kama yupo ndani ya chumba cha mahakama, aliweza kumtambua jirani yake huyo kwa kumnyooshea kidole ili hakimu amuone.

Akijibu maswali ya wakili wa mshitakiwa, Careen amedai alimkuta mume wake chini akiwa ana majeraha kichwani, begani, mgongoni na mguuni na pia jirani aliyowakuta eneo hilo hawakuniambia ambacho kilimpata mume wake.

Baada ya pande zote kumaliza kumuuliza shahidi maswali, Wakili Jafari aliiomba mahakama kufunga ushahidi wao, ambapo Hakimu Rweikiza alikubaliana na ombi hilo na kusema ushahidi wa jamhuri umefungwa rasmi.

Upande wa utetezi, umedai kuwa utawasilisha kwa njia ya maandishi kama mteja wake (mshitakiwa) kama ana kesi ya kujibu au la, ambapo uliomba upewe siku 10 kuanzia tarehe 2.

Hakimu Rweikiza aliahirisha kesi hiyo hadi Aprili 15, 2024 kwa ajili ya kutoa uamuzi kama mshitakiwa ana kesi ya kujibu au la na pia upande utatakiwa kuwasilisha mahakama hapo hoja zao Aprili 9 mwaka huu.

Masahi anayetuhumiwa kumpiga na nyundo jirani yake Minja baada ya kwenda kumshitaki Serikali za Mitaa kwamba anatilisha maji machafu mbele ya nyumba yake.

Katika ushahidi wake, Minja alidai kuwa tarehe hiyo saa mbili na nusu usiku alikuwa akipita nje ya geti la jirani yake Masahi, alimkuta kijana wa jirani huyo, baada ya kumuona alizungumza kwa kilugha kwa sauti kubwa ambae yeye hakuielewa.

By Jamhuri