Na Mwandishi Wetu, Jamhuri Media,
Arusha

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Kanda ya Kaskazini Godbless Lema amesema anasikitika kuona viongozi wa dini kuwa kimya huku vitendo vya utekaji vikiendelea nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Arusha, Lema amewataka viongozi hao kufanya kazi zinazompendeza Mungu ikiwemo kuhakikisha kila binadamu anapata haki yake ya msingi ya kuishi.

Hata hivyo ameitaka jamii kujikita katika mambo ya msingi yenye kuleta mustakabali mzuri wa maisha yao ikiwa ni pamoja na kupinga kwa nguvu zote vitendo vya utekaji watu.

“Mko wapi Mashekhe, mko wapi Maaskofu, mko wapi wachungaji, mko wapi wasanii na wananchi wengine mnaoguswa na matukio haya yanayotishia uhai wa wananchi wasio na hatia? amehoji na kuendelea.

“Hali ni mbaya na kama hatua hazitachukuliwa kuanzia sasa tunakoenda ni kubaya zaidi….watoto, vijana wanatekwa, wengine wanaokotwa wamekufa lakini cha kushangaza hakuna kauli ya serikali yenye majibu kwa nini matukio ya namna hii yanazidi kuongezeka” amesema Lema.

Kwa upande wake Mchungaji wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Kati Usharika wa Olosiva jijini Arusha, Ibrahim Loivotoki amesema kwa upande wake kama Kiongozi anayeongoza kundi kubwa la watu jukumu lake ni kuhubiri amani, upendo mshikamano na utulivu katika jamii.

Pia ameiomba Serikali kuchukua hatua kali kwa wale watakaobainika wakijihusisha na vitendo vya ubakaji, ulawiti na utekaji ili kuhakikisha vitendo hivyo vinakoma na kuweka amani na utulivu kwa wananchi.

“Niwakumbushe wananchi kutoa taarifa na ushirikiano kwa Jeshi la Polisi pindi mnapobaini vitendo vya ukiukwaji haki za binadamu katika jamii zetu zinazotuzunguka na tuwe na hofu ya Mungu siku zote” amesema Mchungaji Ibrahim.

Mkazi wa Kata ya Moshono ambaye hakutaka jina lake litajwe amesema vitendo vya utekaji ni uvunjifu wa amani, hivyo Serikali iwajibike kukomesha vitendo hivyo ili wananchi waendelee kujenga uchumi wao.

“Sasa hivi tunaishi kwa hofu kubwa, watoto wanatekwa, watu wanachinjwa wanatolewa viungo hali inatisha na inatia hofu, tunaitaka serikali itupe majibu juu ya wanaotekwa na kuuawa” amesema mama huyo.

Please follow and like us:
Pin Share