Mkurugenzi Msaidizi wa Kituo cha oparesheni na mawasiliano ya dharula kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na uratibu Bw. Prudence Consintatine 

Viongozi mbalimbali wakishiriki hafla ya kukabidhi miundo mbinu ya vichanja vya kukaushia dagaa 

Mkurugenzi wa Kituo cha mafunzo cha Kanda ya ziwa Mwanza Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini profesa Juvenal Nkonoki.
Muonekano wa vichanja vya kukaushia dagaa

 …………………………………………………………………

Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Mwanza

Mkurugenzi Msaidizi wa Kituo cha Operesheni na Mawasiliano ya Dharura Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Prudence Constantine amevitaka vikundi vya ushirika vya wachakata dagaa vya Wilaya za Pangani na Bagamoyo kutumia miundombinu ya kudumu ya kukaushia dagaa kuongeza thamani ya bidhaa hiyo. 

Ametoa rai hiyo Ijumaa Novemba 17, 2023 katika hafla ya kukabidhi miundombinu ya kudumu ya vichanja vya kukaushia dagaa kwa kikundi cha Simama Wanawake na Maendeleo (SIWANA) cha Wilayani Bagamoyo Mkoani Pwani. 

Constantine amevihimiza vikundi hivyo vya ushirika kutumia miundombinu hiyo ya kukaushia dagaa kupata dagaa wenye ubora wa hali ya juu ili kukidhi ubora wa soko la Kimataifa.

“Nitumie fursa hii kuwahimiza wanaushirika wa SIWANA wa hapa Wilayani Bagamoyo na Chama cha Ushirika cha Wavuvi na Wafanyabiashara wa Mazao ya Uvuvi (UWABIMAU) wa Kata ya Kipumbwi Wilayani Pangani kutumia miundombinu hii tunayowakabidhi hii leo na mingine iliyokabidhiwa jana Novemba 16, 2023 kule Wilayani Pangani ikawawezeshe kupata dagaa bora watakao weza kukidhi soko la Kimataifa na kuwezesha ushirika wenu kukua kiuchumi” amesema Bw. Constantine.

Wakati huo huo Mwenyekiti wa Halmashauri ya Bagamoyo Mohamed Usinga akitoa salamu za wanufaika wa mradi amewashukuru Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) pamoja na Serikali ya Japani kupitia ubarozi wake Nchini Tanzania kwa ufadhili wa ujenzi huo wa miundombinu ya kukaushia dagaa na ameahidi kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo itaendelea kuviunga mkono vikundi vyote vya ushirika vilivyopo wilayani hapo.

Aidha, Mkurugenzi wa Kituo cha Mafunzo cha Kanda ya Ziwa – Mwanza, Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini Prof. Juvenail Nkonoki akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo amesema Chuo kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) walianza uratibu wa utekelezaji wa malengo ya mradi wa kukabiliana na vitendo vya kihalifu katika Bahari na Maziwa Makuu Nchini ambapo Mwezi Septemba 2023 yalifanyika mafunzo maalumu ya kuvijengea uwezo  juu ya  misingi ya ushirika na kujitegemea kwa vikundi vilivyopo Bagamoyo, Pangani na Mafia.

 “Kwa sasa Chuo kinaendelea na kufanya upembuzi yakinifu na kuandaa andiko la kupata mitambo ya kisasa ya kuchakata Dagaa mradi utakao gharimu takribani Shilingi Billioni 1.2” amesema Profesa Nkonoki.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Emmanuel Nnko amesema kuwa shirika litaendelea kushirikiana na vikundi vya ushirika na Serikali kwa hatua zaidi kwa kutengeneza mnyororo wa thamani wa mazao ya baharini.

“Hii ilikuwa hatua ya kwanza kwa kuwatoa wachakata dagaa kwenye kuanika chini kwenda kuanika kwenye vichanja,hatua ya pili ni kutoka hapa kwenda kwenye kiwanda cha kuchakata dagaa baada ya andiko la mradi kukamilika” amesema Bw. Nnko

Ujenzi wa Miundombinu hii ya kuanikia dagaa ni moja kati ya malengo ya mradi wa kukabiliana na vitendo vya kihalifu katika Bahari na Maziwa Makuu Nchini, ambapo Mwezi Februari 2023 Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb) alizindua Mwongozo wa kukabiliana na vitendo vya kihalifu katika Bahari na Maziwa Makuu Nchini kwa lengo la kuimarisha ulinzi na usalama katika maeneo hayo, na Mwezi Septemba 2023 yalifanyika mafunzo ya kuwajengea uwezo Wavuvi na Wachakataji wa dagaa katika Wilaya za Mafia, Pangani na Bagamoyo ambapo walijengewa uwezo  juu ya  misingi ya ushirika

By Jamhuri