Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia,Dodoma

ZAIDI ya Wananchi 152 wa Mitaa ya Chimala na Ntyuka Jijini Dodoma wamelalamikia Wakala wa Barabara nchini (TANROAD )Mkoa wa Dodoma kwa kutolipwa fidia baada ya kupisha ujenzi wa Barabara licha ya Wakala huo,kuwafanyia uthamini tangu Mwaka Jana na kuahidi kuwalipa fidia ifikapo mwezi juni Mwaka huu.

Hatua hii imetokana na Wananchi wa Mitaa hiyo miwili ya Chimalaa na Ntyuka kupisha ujenzi wa Barabara ambayo inaanzia Kata ya Ntyuka kuelekea Kata ya Kikombo Jijini Dodoma,yenye urefu wa jumla ya Kilomita 76.

Kutokana na hayo wamemuomba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk.Samia Suluhu Hassan kuingilia kati suala hilo ili wapate stahili zao na kuendelea na shughuli zao bila kadhia yoyote.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma, Mmoja wa wananchi hao Michael Tengo ameeleza kuwa kabla ya ujenzi wa Barabara hiyo kuanza, waliahidiwa na wakala huo kulipwa fidia kabla ya ujenzi jambo ambalo halija tekelezwa hadi sasa.

“Tunaomba Rais wetu mpendwa atusaidie hili,Shughuli zetu za uzalishaji zimesimama kwa muda mrefu na hatujui hatma yetu, na juzi walikuja kutuambia tunapaswa kubomoa nyumba zetu kwa hiari hili jambo linatuumiza sana,” Amesema

Naye Lightness Nkya ameeleza kuwa huenda kero hiyo ikawa inasababishwa na uongozi wa eneo hilo kutokana na kutokuwa na ushirikiano wa moja kwa moja na wananchi ambapo Mtendaji wa Kata hiyo Mara nyingi akiiulizwa kuhusu fidia hukataa kuzungumzia suala hilo.

“Mtendaji wa Mtaa huu hataki kutushirikisha shughuli za maendeleo nadhani hii ndo sababu ya kuzalisha Migigoro isiyoisha, inawezekana kabisa labda suala hili kisingefikia hapa kama angetupa ushirikiano, hata tukimuuliza mambo yanavyoendelea huwa anakataa na kutueleza kuwa yeye siyo mhusika,” amesema.

Amesema, “Kwa hiyo naamini watu wengi wamekuwa wakilalamikia Serikali kwa mambo mengi bila kujua watendaji wake wa chini ndiyo wanaoiangusha, tunaomba Serikali iangalie hili watu ambao imewaamini kuwa ni wawakikishi wake huku chini hawatusaidii sisi wanyonge, ” Amesisitiza

Kwa upande wa Mwenyekiti wa kamati ya ufuatiliaji wa malipo ya fidia Athanas Matonya ameeleza kuwa mbali na madai hayo yapo madai mengi ambayo wananchi hao wanadai fidia kwa muda mrefu bila kulipwa.

Amesema, “Wananchi wanadai fidia kwenye eneo la Udoma na Chuo cha mwalimu Nyerere ambapo maeneo yamechukukiwa bila kulipwa, tunashangaa wenzetu wa Iyumbu na Nghonghonha wamelipwa lakini sisi hatujalipwa, ” amesema.

Mbali na hayo amesema Mradi huo ambao ulianza mwezi Agosti Mwaka 2022 ulipaswa kuanza baada ya malipo ya fidia yao na kwamba serikali inapaswa iwaelekeze nini cha kufanya na ikiwa haiwezekani kuwalipa basi wananchi waelezwe bila fuwaficha.

Akizungumzia kuhusiana na suala hilo,Diwani wa Kata ya Ntyuka,Yona Endrew amesema amefuatilia suala hilo kwa Wakala wa Barabara Mkoa wa Dodoma (TANROAD) ambao umekuwa ukitoa ahadi ya kuwalipa wananchi hao lakini haujatekeleza.

Ameeleza kuwa Wananchi hao kwa sasa hawajui ni lini watapata stahiki zao na kubaki na sintofahamu kutokana na Ujenzi huo wa Barabara kuendelea bila wao kujulishwa lolote na hivyo kudhani kuwa huenda wamezulumiwa haki yao.

“Wananchi hawa unaowaona hapo ni katika wana kilio cha muda mrefu takribani Mwaka mmoja Sasa tangu waahidiwe kulipwa fidia kutokana na kusimamisha shughuli mbalimbali ikiwemo kilimo baada ya maeneo yao kuchukuliwa na Serikali,hivi Sasa wanadai kuambiwa waondoke na wengine kubomoa Nyumba zao bila ya kujua hatima yao, “amesema.

Naye Mhandisi toka Wakala wa Barabara Mkoa wa Dodoma( TANROAD)Calman Gaston,akizungumza na Wananchi hao,kwa niaba ya Meneja wa Wakala huo Mkoa wa Dodoma,amewaahidi wananchi hao kuwa wavumilivu kwani watalipwa stahili zao jambo ambalo liliwafanya wananchi hao kukataa kauli hiyo na kusema kuwa ni uongo kutokana na ahadi hizo kutokewa kila siku bila utekelezaji na kugoma kuondoka katika Ofisi za Kata ya Ntyuka wakishinikiza Meneja wa TANROAD aende kuwalipa fidia zao.

Hata hivyo juhudi za Meneja huyo wa TANROAD kufuka katika eneo hilo bado hazikufanikiwa kutokana na kueleza kuwa bado anaendelea na majukumu mengine ya Kiserikali.

By Jamhuri