Na Mwandishi Wetu JAMHURI MEDIA Dar es Salaam.

Viongozi wa Afrika wamekusanyika leo Septemba 08, 2023 Dar es Salaam Tanzania ikiwa ni kilele kama sehemu ya Jukwaa la Mifumo ya Chakula Afrika 2023.

Jukwaa hilo lililohitimishwa leo mchana limekusanya zaidi ya wajumbe 5000 kutoka kote duniani kwa lengo la kuchunguza sera, mafanikio na ubunifu utakaoharakisha mabadiliko ya mifumo ya chakula barani Afrika.

Katika mkutano huo, Wakuu wa Nchi kutoka Tanzania, Kenya, Burundi, Senegal na Zanzibar zimejadiliwa hatua mbalimbali ambazo nchi zao zinatekeleza ili kubadilisha mifumo yao ya chakula kwa lengo la kukabiliana na uhaba wa chakula na kuimarisha ustahimilivu.

Katika hotuba yake ya ufunguzi Hassan, rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan amesisitiza dhamira ya Tanzania katika kuleta mapinduzi kwenye sekta ya kilimo ili kuibuka kuwa mzalishaji mkuu wa chakula barani Afrika.

“Ninaamini kuwa Afrika inaweza kulisha dunia na serikali yangu imeongeza bajeti ya kilimo karibu mara nne, katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, kutoka dola za Marekani milioni 120 mwaka 2021/2022 hadi dola milioni 400 mwaka 2023/24 katika jitihada za kuchochea kilimo na mageuzi ya mfumo wa chakula nchini Tanzania,” alisema.

Rais Samia amewataka viongozi wa Afrika kuendana na Azimio la Malabo ambalo linayaamuru mataifa ya Afrika kutenga kima cha chini cha asilimia 10 ya bajeti zao kwa kilimo, ikilenga angalau asilimia sita kwa kiwango cha ukuaji wa kila mwaka.

Akizungumza katika hafla hiyo, Hailemariam Dessalegn, ambaye ni Waziri Mkuu wa zamani wa Ethiopia na Mwenyekiti wa Kikundi cha Washirika wa AGRF aliangazia maswala muhimu yanayokabili Mifumo ya Chakula ya Afrika ikiwa ni pamoja na mzozo unaoendelea wa Urusi na Ukraine, athari mbaya za janga la COVID-19, kuongezeka kwa ukame na mafuriko, usumbufu wa usambazaji, migogoro na masuala mengine muhimu.

“Tuko katika harakati za kupona kutokana na mishtuko mitatu mikuu na hitaji la hatua ya kuleta mabadiliko halijawahi kuwa la dharura zaidi. Jukwaa la Mifumo ya Chakula barani Afrika 2023 ni wakati mahususi wa kuangazia na kufungua ahadi za bara hili za kisiasa, sera na kifedha na ubunifu kuelekea kufikia mifumo yenye tija, yenye lishe, jumuishi, inayostahimili na endelevu ya chakula barani Afrika,” amesema.

Mkutano huo uliowaleta pamoja maelfu ya washiriki pamoja na watu wengine mashuhuri akiwemo Waziri Mkuu wa Zamani, wa Jamhuri ya Benin;Lionel Zinsou, Dkt Jakaya Kikwete, Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jonathan Goodluck, Rais wa zamani wa Nigeria na Mohamed Beavogui, Waziri Mkuu wa zamani wa Guinea.

By Jamhuri