Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi nchini Kenya Francis Ogolla amefariki.

Rais William Ruto ametangaza kifo cha Ogolla pamoja na maafisa wengine tisa wa jeshi huku wawili wakinusuruka.

Ogolla alifariki baada ya helikopta aliyokuwa akisafiria pamoja na maafisa wengine kuanguka Kaben, Marakwet Mashariki siku ya Alhamisi.

Ogolla alichukua nafasi ya kuongoza jeshi mnamo Aprili 28, 2023.

Walioshuhudia walisema kuwa ilishika moto wakati wa kuanguka. Eneo hilo lilizingirwa mara baada ya ajali hiyo.

Maafisa hao walikuwa wakichunguza eneo hilo kabla ya kutumwa kwa wanajeshi zaidi kukabiliana na wezi wa mifugo katika eneo hilo.

Helikopta hiyo ya Jeshi la Anga la Kenya aina ya Huey ilikuwa imetoka katika shule moja ya msingi ya eneo hilo ilipoanguka na kuwaka moto.

Ogolla aliteuliwa kuwa Mkuu mpya wa Majeshi ya Ulinzi katika mabadiliko katika jeshi, akichukua hatamu kutoka kwa mtangulizi wake Jenerali Robert Kibochi.

Kibochi alimkabidhi Ogolla kama Mkuu wa majeshi baada ya kufikisha umri wa kustaafu .

By Jamhuri