Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia,Dar

Taasisi ya Mo Dewji Foundation iliyoanzishwa na mfanyabiashara Mohamed Dewji, imetoa msaada wa Sh100 milioni kwa ajili kusaidia matibabu ya watoto wanaosumbuliwa na Saratani.

Akikabidhi msaada huo leo jijini Dar es Salaam kwa Taasisi ya Tumaini la Maisha iliyopo katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Mkurugenzi wa Mo Dewji Foundation, Rachel Carp amesema msaada huo unalenga kuboresha afya na kurejesha tumaini kwa wagonjwa.

Rachel amesema mbali na kutoa msaada huo wa kifedha wametoa sabuni za kufulia, kuogea na khanga ambazo wanaamini ni miongoni mwa mahitaji muhimu kwa wahusika.

“Taasisi ya Mo Dewji inaangazia elimu, maendeleo ya jamii, afya na uwezeshaji wa kijinsia. Tunaamini kuwa huduma bora za afya zinazopatikana ni haki kwa binadamu, na tumejitolea kuboresha huduma za afya hapa Tanzania” amesema.

Amesema tangu mwaka 2013, wameshirikiana na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kupitia Tumaini la Maisha, Kituo Kikubwa zaidi cha Saratani ya Watoto Afrika Mashariki.

Rachel amesem wanaendelea kufanya kazi na Tumaini la Maisha kwa sababu programu zao ni muhimu kwa maisha ya watu wa nchi za Afrika Mashariki.

Janeth Mashauri na Frank kinabo kutoka Taasisi ya Mo Dewji Foundation, wakimkabidhi Dk. Gerald Mongella, Mwenyekiti wa Bodi ya taasisi ya Tumaini la Maisha mfano wa hundi ya Shilingi milioni 100. Ikiwa ni mwendelezo wa ushirikiano baina ya Taasisi ya Mo Dewji na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kupitia Taasisi Tumaini la Maisha kusaidia matibabu ya watoto wenye saratani Tanzania.

“Programu zao hutoa huduma za kiafya na zisizo za kiafya kwa watoto, kama vile ununuzi wa dawa za Kemotherapy, usaidizi kwa programu ya shule, matengenezo ya mpango wa usafiri kwa wagonjwa na walezi wao, usaidizi wa programu ya tiba ya michezo kwa wagonjwa, usaidizi katika mafunzo ya stadi za maisha kwa wazazi, vifurushi kwa wagonjwa wapya waliolazwa, na usaidizi wa mshahara kwa wafanyakazi ambao sio wa afya” amesema.

Ametoa wito kwa Watanzania wote kuunga mkono juhudi muhimu za Tumaini la Maisha na mashirika mengine yasiyo ya kiserikali yanayojishughulisha na kuwawezesha watu wengi wasiojiweza nchini Tanzania.

Akizungumza mara baada ya kupokea msaada wa sabuni za kufulia, kuogea na khanga, Eliza Sanga ambaye ni mzazi wa mtoto anayepata matibabu ya Saratani katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili amesema msaada huo ni mkombozi kwao na kuwaomba Watanzania wengine kuiga moyo wa kujitolea kama walivyofanya Mo Dewji Foundation.

“Tuna mahitaji ya muhimu mengi na baadhi yetu hatuna uwezo hivyo tunaposaidiwa tunafarijika zaidi” amesema.

Akipokea mfano wa hundi ya Sh100 milioni,Mwenyekiti wa Bodi ya taasisi ya Tumaini la Maisha, Gerald Mongella amesema Mo Dejwi Foundation wameonyesha mfano mzuri wa kusaidia jamii yenye uhitaji hivyo amewaomba Watanzania wengine wahasike kusaidia matibabu ya watoto wenye saratani.

“Serikali peke yake haiwezi kufanya kila kitu kwa kiwango ambacho kila mmoja anakihitaji lakini kwa ushirikiano wa wadau mbalimbali malengo husika hufikiwa na jamii yenye shida hupata faraja” amesema.