Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia, Dodoma.

Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI),ipo mbioni kuanzisha huduma ya kutibu ugonjwa wa kifafa kwa njia ya upasuaji na utengenezaji wa mkono wa umeme ambapo wagonjwa watano wameshahudumiwa.

Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Profesa. Abel Makubi amesema hayo leo Agosti 3,2023 Jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa majukumu yake na kufafanua kuwa huduma hizo zitasaidia kuboresha afya ya watanzania.

Alifafanua kuwa kwa wananchi ambao tayari wamewekewa mikono hiyo imewasaidia kufanya baadhi ya shughuli ambazo wasingeweza kuzifanya.

“Taasisi imeanzisha huduma mpya ya utengenezaji wa mkono wa umeme ambapo tayari wagonjwa watano wameshahudumiwa., Gharama zake ndani ya nchi ni sh. milioni 15 na nje ya nchi ni milioni 30 hadi 60, hii hudumani mpya, tuliwapeleka madaktari kwenda kusoma na tutaendelea kutoa kwa wananchi wengi zaidi wenye uhitaji,”amesema

Profesa. Makubi amesema huduma za karakana ya viungo bandia MOI, zimeendelea kuimarika ambapo katika kipindi cha miaka miwili ya uongozi wa Rais Dk.Samia Suluhu Hassan viungo bandia 555 vimetengenezwa.

Kuhusu huduma za kibingwa Profesa. Makubi ameleza kuwa MOI imepanga kuanzisha huduma mpya tatu za kibingwa ambazo ni tiba ya kiharusi, tiba ya kifafa kuputia upasuaji na upasuaji wa kiuno kwa njia ya matundu.

Amesema lengo la kuanzisha huduma hizo ni kutokana na magonjwa hayo bado ni changamoto na kusababisha wagonjwa kupewa rufaa nje nchi.

“Katika mwaka huu wa fedha, serikali imetenga sh.bilioni 55.9 kwa MOI ili kuboresha huduma za tiba na shughuli za uendeshaji, tumepanga kuanzisha huduma mpya tatu za kibingwa ambazo bado zinasababisha rufaa nje nchi.

By Jamhuri