Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia,Pwani

Watu wanne wamefariki baada ya gari walilokuwa wakisafiria kugonganga uso kwa uso na gari aina ya Scania katika Kijiji cha Mapatano,kata ya Mbwewe Wilaya ya Kipolisi Chalinze.

Ajali hiyo inaelezwa kwamba ilitokea saa 8.30 usiku wa kuamkia Agost 3, mwaka huu ,ambapo gari yenye namba za usajili T 104 CBU Toyota Prado ikitokea Dar es Salam kwenda Same ikiendeshwa na Nechi Msuya aliyekuwa Mkurugenzi wa benki ya APSA iligongana na Lori.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani Pius Lutumo alieleza kwamba gari hiyo ikiendeshwa na Msuya anayekadiriwa kuwa na umri wa (45-50) iligongana na gari yenye namba za usajili T 881 DWU/ T 888 DWU aina ya scania ikiendeshwa na dereva Philipo Mtisi (43) ikitokea Arusha kwenda Dar es Salam.

Amewataja waliofariki katika ajali hiyo kuwa ni dereva wa Toyota Prado Nechi Msuya, Dayana Mageta, Nora Msuya ambaye alikuwa mwalimu wa Chuo Kikuu cha Mzumbe tawi la Dar es Salam na abiria mwingine wa kike anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 30-35 jina halijafahamika.

Kamanda Lutumo amesema chanjo cha ajali hiyo ni dereva wa Toyota Prado kuhama kutoka upande wa kushoto kwenda kulia kisha kugongana uso kwa uso na Lori hilo.

Miili ya waliofariki katika ajali hiyo imehifadhiwa katika Zahanati ya Lugoba ikisubiri uchunguzi wa daktari na kukabidhiwa kwa ndugu kwa mazishi.

Vilevile ametoa wito kwa madereva na watumiaji wa barabara kuchukua tahadhari na kuzingatia sheria za usalama kuepukana na qjali zinazoweza kusababishwa na uzembe.

Hata hivyo, madereva wa vyombo vya moto wetahadharishwa kutumia vileo wanapoendesha vyombo vya moto kwani imekuwa chanzo cha kusababisha ajali za barabarani.

By Jamhuri