Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia

Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI) kwa kipindi cha mwaka mmoja imefanikiwa kufanyia upasuaji wa kibingwa wagonjwa 7113 wa tiba ya mifupa ikiwa ni idadi kubwa ukilinganisha na wagonjwa 6793 katika mwaka uliopita huku wagonjwa wa ajali za barabarani wakiongoza.

Hayo yameelezwa leo Julai 29,2022 jijini Dodoma na Mkurugenzi wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI) Dk. Respicious Boniface,wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekekezaji wa shughuli za taasisi hiyo na mwelekeo wa utekekezaji kwa mwaka wa fedha 2022/23

Dk.Boniface amesema kuwa taasisi hiyo imeanza mchakato wa kupeleka huduma hizo katika hospitali za kanda na mikoa ili kupunguza msongamano wa wagonjwa katika hospitali hiyo.

Mkurugenzi wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI) Dk. Respicious Boniface, akizungumza na waandishi wa habari leo Julai 28,2022 jijini Dodoma kuhusu utekekezaji wa shughuli za taasisi hiyo na mwelekeo wa utekekezaji kwa mwaka wa fedha 2022/23

”Katika kipindi cha mwaka mmoja jumla ya wagonjwa 7,113 walifanyiwa upasuaji ikilinganishwa na wagonjwa 6,793 waliofanyiwa katika mwaka uliopita wa 2020/2021 ikiwa ni ongezeko la asilimia 2.

“Upasuaji mbalimbali wa kibingwa uliofanyika ni pamoja na kubadilisha nyonga 207 kubadilisha magoti 182 upasuaji wa mfupa wa kiuno 96, Wagonjwa 200 wamefanyiwa upasuaji wa magoti na mabega kwa njia ya matundu (Knee and Shoulder athroscopy) kati yao waliofanyiwa mabega ni 32 na magoti ni 168, wagonjwa 249 wamefanyiwa upasuaji wa uti wa mgongo kwa kufungua eneo dogo (minimal invasive spine surgery)”amesema.

Dk. Boniface, amesema kuwa majeruhi wengi ni wa ajali za pikipiki (bodaboda) pamoja na magari huku akiwataka Watanzania kuzingatia sheria za usalama barabarani ili kuipunguzi mzigo serikali wa kuhudumia majeruhi hao.

“Kama Taasisi tumekuwa tukiwahudumia wagonjwa hawa wa ajali za Bodaboda kwa aliyevunjika mfupa gharama ni Shilingi milioni 1.5 lakini akiumia kichwa akakaa ICU gharama yake ni Shilingi milioni tano hadi sita na akikaa miezi mitatu hapo gharama ndipo inakuwa kubwa hadi kufikia Shilingi Milioni 30.

“Wagonjwa hawa wa ajali za Bodaboda wengi hawana bima na wana hali za chini za kimaisha kwahiyo huwa ni changamoto na kupelekea wengine kutelekezwa wodini na familia zao,”alisema Dk.Boniface

Aidha Dk.Boniface amesema kuwa Serikali imetoa Sh. bilioni 4.2 kwa ajili ya ununuzi wa ‘Implants’ ili kukabiliana na changamoto ya uhaba wa implants kwa wagonjwa.

“Vifaa hivi vimesaidia kuendelea kuboresha huduma za matibabu ya kibingwa ya Mifupa, Ubongo, Uti wa mgongo na Mishipa ya Fahamu, hivyo kuokoa maisha ya Watanzania wengi na pesa za serikali ambazo zingetumika kupeleka wagonjwa nje ya nchi kwa matibabu”amesema Dkt. Boniface

Pia katika kipindi hicho cha mwaka mmoja watoto 17 wamefanyiwa upasuaji wa kunyoosha vibiongo (scoliosis) Wagonjwa 11 wamefanyiwa upasuaji wa kuondoa vivimbe vya mishipa ya damu kwenye ubongo (celebral aneurysm repair).

Katika hatua nyingine Dkt. Boniface amesema taasisi itaendelea kutoa huduma bora na itaendelea kushirikiana na taasisi za mataifa mengine katika kuendeleza taaluma hiyo.

By Jamhuri