Na Aziza Nangwa,JamhuriMedia

Huduma za kibingwa za Taasisi ya tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI) zitaanza kutolewa katika hospitali mpya na ya kisasa ya rufaa ya kanda Mtwara ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Serikali la kusogeza huduma za kibingwa karibu na wananchi.

Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanali Ahmed Abbas Ahmed amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha ujenzi wa hospitali ya rufaa ya kanda Mtwara ambayo itahudumia wakazi wa mikoa ya Mtwara, Lindi, Ruvuma pamoja na mataifa jirani.

“Hospitali hii haitahudumia wakazi wa mikoa ya kusini peke yake, tunatarajia wagonjwa kutoka Msumbiji, Komoro na hata Malawi, hivyo ujio wa huduma za MOI utachagiza utalii wa matibabu hapa na kubwa zaidi ni huduma zimesogezwa karibu na wananchi pasipo kulazima kufuata huduma hizo Dar es Salaam” amesema Kanali Ahmed

Kanali Ahmed amesema Serikali ya Awamu ya Sita imetoa fedha kwaajili ya ununuzi wa vifaa vya kisasa katika hospitali hiyo ambapo mtambo wa kisasa wa CT-Scan umeshawasili kwaajili ya usimikaji, mashine ya X-ray imeshasimikwa na mashine ya kisasa ya MRI itawasili hivi karibuni.

Kwa upande wake Katibu tawala wa Mkoa wa Mtwara Abdallah Malela amemshukuru Mkurugenzi Mtendaji wa MOI Dkt Respicious Boniface kwa mwitikio wake wa kufika Mtwara ili kuona namna bora ya kushirikiana na Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mtwara katika kuanzisha huduma za kibingwa za Mifupa.

Mkurugenzi Mtendaji wa MOI Dkt Respicious Boniface amasema MOI inatekeleza kwa vitendo agizo la Mh Rais Samia Suluhu Hassan la kuhakikisha huduma za kibingwa za Mifupa, Ubongo, Mgongo na Mishipa ya Fahamu zinazogezwa karibu na wananchi ambapo katika mikoa ya kusini tayari huduma za MOI zinapatikana katika hospitali za Nyangao Lindi pamoja na Ndanda.

By Jamhuri