Na Tatu Saad,JamhuriMedia

Baada ya ushindi mnono wa mabao 7-0 walioupata Simba Sc dhidi ya Horoya ya Guinea katika mchezo wa mzunguko wa tano wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika,leo Yanga Sc wanakutana na US Monastir ya Tunisia katika dimba la Benjamin Mkapa.

Yanga inatarajia kukutana na US Monastir katika mchezo wa mzunguko wa tano wa kombe la shirikisho Afrika katika uwanja wa nyumbani Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.

Kuelekea mchezo huo utakaopigwa leo saa moja kamili usiku, kocha mkuu wa US Monastir Darko Novic amesema kuwa katika mchezo wa leo hawatatumia nguvu kubwa kuwakabiri Yanga SC kwani wao tayari wa Kesha Una hatua ya robo fainali.

“Hatukuja Tanzania kutafuta alama tatu wala suluhu kwa sababu tumeshafuzu Robo Fainali, hivyo tutacheza mpira wa kawaida bila ya kutumia nguvu nyingi kama tulivyocheza nao Tunisia.” amesema Novic

Hata hivyo Novic amesema kuwa kikosi chake kipo tayari kuwakabiri Yanga lakini amewasihi wachezaji wake kucheza kwa makini ili kujiepusha na majeraha.

“Tunafahamu wapinzani wetu wanahitaji ushindi ili wafuzu hatua inayofuatia ya Robo, hivyo tayari nimewaambia wachezaji wacheze kwa makini ili wamalize mchezo huo bila ya majeraha yoyote.” Amesema Novic.

Vile vile kocha msaidizi wa Yanga SC, Cedric Kaze amesema kazi maalum ya ukimaliza US monastir wamewakabidhi washambuliaji wao mahiri Fiston Mayele na Kennedy Musonda.

Pia Kaze amesema wapo tayari kuhakikisha wanapata ushindi katika mchezo huo ambao pia utakuwa ni mchezo wa kisasi baada ya kupoteza kwenye mzunguko wa kwanza wa kombe la shirikisho huko Tunisia.

Aidha Kaze amesema wamewandaa vyema wachezaji wao kimbinu na kuwapa maelekezo ya majukumu yao ambayo wakiyatimiza kwa ufasaha watapata ushindi wa kupeleka robo fainali.

“Hatuwaogopi licha ya wapinzani wetu wana timu nzuri, walitufunga kwao na sisi tuna uwezo wa kuwafunga hapa Tanzania, tunaendelea kujipanga ili tushinde na naamini tutafanya hivyo kama kila kitu kitaenda tulivyopanga.” amesema Kaze.

Yanga Sc ipo nafasi ya pili katika msimamo wa kundi D wa kombe la shirikisho barani Afrika wakiwa na alama saba huku wapinzani wao US Monastir wakiongoza kundi kwa alama 10.

By Jamhuri