Na mwandishi wetu

Saa 12:00 jioni ya leo waafrika wengi watakuwa mbele ya televisheni zao wakiangalia mechi ya Kombe la Dunia kati ya Morocco na Canada kwa matumaini makubwa ya kuona timu nyingine toka Afrika ikifuzu hatua ya 16 Bora kwenye Kombe la Dunia nchini Qatar na kuungana na Senegal ambao tayari wamefuzu katika hatua hiyo. 

Morocco wanahitaji matokeo ya sare au ushindi ili kufuzu kwenda katika hatua ya 16 Bora ya Michuano ya Kombe la Dunia nchini Qatar ambapo mwaka huu timu nyingi za Afrika zimeonekana kufanya vizuri hata zile ambazo zimetolewa hazikutolewa kinyonge. 

Morocco wapo katika nafasi ya pili kwenye kundi F wakiwa na alama 4 sawa na Croatia wanayeongoza kundi hilo wakitofautiana kwa idadi ya magoli ya kufunga na kufunga. 

Croatia watakuwa wanavaana na Ubelgiji wenye alama 3. Ubelgiji wanahitaji ushindi ili kufuzu kwenda hatua ya 16 Bora wakati Croatia watakuwa wanahitaji walau matokeo ya sare tu na kufuzu kwenda hatua hiyo inayofuata. 

Morocco wanakutana na Canada ambao wamepoteza mechi zote na hawana alama hata moja katika michuano hiyo. Kocha wa Morocco Walid Regragui amesema timu yake inahitaji kuchukua tahadhari zote kwa sababu wanakutana na timu ambayo itacheza bila presha yeyote ya matokeo.

By Jamhuri