Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango amelitaka Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) pamoja na Mamlaka za Serikali za Mitaa kote nchini kuongeza nguvu zaidi katika kusimamia utekelezaji wa katazo la matumizi ya mifuko ya plastiki hapa nchini.

Makamu wa Rais ametoa maagizo hayo mara baada ya kuongoza zoezi la kufanya usafi katika soko kuu la wamachinga mjini Dodoma ikiwa ni katika kuadhimisha Siku ya Mazingira Duniani leo tarehe 5 Juni 2023. Amesema ni lazima kuhakikisha hatua za kisheria zinachukuliwa kwa wanaokiuka maagizo hayo pamoja na kuwataka watendaji wote wanaohusika kusimamia kwa karibu uzalishaji na matumizi ya mifuko mbadala.  

Makamu wa Rais ameongeza kwamba ni vema kuhakikisha mifuko yote inayozalishwa inaonesha taarifa za mzalishaji na kama inakidhi viwango vilivyowekwa na mamlaka husika. Pia amesisitiza makampuni na watu binafsi wanaozalisha bidhaa za plastiki kuhakikisha taka zinazotokana na bidhaa zinazozalishwa zinakusanywa na kuondolewa.

Halikadhalika Makamu wa Rais amezitaka Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhakikisha kampuni zinazopewa kazi ya kuzoa taka ziwe na uwezo kufanya kazi hizo kwa ufanisi. Amekemea utoaji wa tenda za uzoaji taka kwa kampuni zisizokuwa na uwezo na zile zisizo na vitendea kazi vya kisasa na kuzitaka Halmashauri kuweka miundombinu ya uhakika ya ukusanyaji na usombaji wa taka katika mitaa na maeneo ya mikusanyiko kama sokoni, stendi na hospitalini.

Aidha Dkt. Mpango ametoa wito kwa wananchi kutambua wajibu walionao katika kutunza vyanzo vya maji, kuacha mazoea ya kutupa taka hovyo na kuagiza kila kaya kuwa na sehemu mahsusi ya kuhifadhia ama kuchomea taka. Amesema masuala ya kufanya usafi na utunzaji mazingira hayana mbadala kwa kuwa mazingira ndio uhai na yana mahusiano ya moja kwa moja na ustawi wa Taifa kiuchumi na kijamii.

Kwa upande wake amesema suala la utunzaji na uhifadhi wa mazingira limeendelea kupewa kipaumbele hapa nchini ambapo kwa kutumia Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa kauli mbiu iliopo ni yenye lengo la kuhamasisha ajenda ya utunzaji wa mazingira na kutunza vyanzo vya maji.

Dkt Jafo amewapongeza wanafunzi kuanzia shule za msingi hadi vyuo vikuu kwa kujitoa kihifadhi mazingira ikiwemo kampeni ya soma na mti yenye lengo la kuhamasisha upandaji wa miti mashuleni. Halikadhalika amewashukuru wadau mbalimbali katika jitihada zao za kuhakikisha suala la mazingira linapewa kipaumbele kwa maendeleo endelevu.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule amesema mkoa huo unaendelea na kampeni ya kudhibiti matumizi ya mifuko ya plastiki ambapo tayari kwa kushirikiana na NEMC waliweza kukifungia kiwanda kimoja kinachozalisha mifuko hiyo. Amesema elimu inaendelea kutolewa katika masoko na maeneo mbalimbali ili kuhakikisha wananchi wanaachana na matumizi ya mifuko hiyo.

Pia ameongeza kwamba Mkoa huo utaendelea na jitihada za kulinda vyanzo vya maji ikiwemo chanzo cha maji Mzakwe kwa kusimamia na kupanda miti katika eneo hilo muhimu. Amesema mkoa utaendeleza hamasa ya usafi wa mazingira iliofanyika katika wiki ya kuadhimisha siku ya mazingira duniani hususani usafi katika mifereji ya jiji la Dodoma.

Zoezi la kufanya usafi katika soko kuu la wamachinga mjini Dodoma limewashirikisha viongozi mbalimbali, wananchi na watumiaji wa soko hilo. Kauli mbiu ya Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani kwa mwaka 2023 inasema “Shinda uchafuzi wa mazingira unaotokana na taka za plastiki”

Share

SHARE

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akiongoza Viongozi na Wananchi mbalimbali wa Mkoa wa Dodoma kufanya usafi katika Soko Kuu la Wamachinga mjini Dodoma ikiwa ni Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani leo Juni 5,2023.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akisukuma toroli alilotumia kukusanya takataka mara baada ya kuongoza zoezi la kufanya usafi katika Soko Kuu la Wamachinga mjini Dodoma ikiwa ni Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani leo Juni 05  2023.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akihutubia Viongozi na Wananchi mbalimbali wa Mkoa wa Dodoma mara baada ya kuongoza zoezi la kufanya usafi katika Soko Kuu la Wamachinga mjini Dodoma ikiwa ni Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani leo tarehe 05 Juni 2023.

By Jamhuri