Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango amesema ushirikiano unahitajika baina ya serikali, sekta binafsi, wadau wa maendeleo, taasisi za fedha za ndani, azaki pamoja na taasisi za elimu na utafiti ili kuitekeleza vema kampeni ya uwekezaji katika sekta ya maji barani Afrika.

Makamu wa Rais amesema hayo alipomwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Mkutano wa uzinduzi wa Kampeni ya Jopo la Viongozi wa Juu kuhusu Programu ya Uwekezaji katika Sekta ya Maji Barani Afrika uliyofanyika kando ya Mkutano wa Baraza Kuu la 78 la Umoja wa Mataifa Jijini New York nchini Marekani.

Ametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kushirikiana na Tanzania katika kukusanya rasilimali fedha ili kukamilisha uwekezaji katika sekta ya maji kwa kuzingatia tayari Tanzania imedhamiria kukusanya takribani asilimia 43 ya rasilimali fedha kutoka katika vyanzo vya mapato ya ndani ili kufanikisha uwekezaji huo.

Makamu wa Rais amesema Tanzania kama moja ya watekelezaji wa programu hiyo imeandaa programu ya uwekezaji katika sekta ya maji (TanWIP) ambayo inatarajiwa kutekelezwa kuanzia mwaka 2024 – 2030. Ametaja malengo ya uwekezaji huo ni pamoja na kuhakikisha usalama wa maji wa Taifa, uhimilivu katika athari za mabadiliko ya tabianchi pamoja na upatikanaji wa maji ya kutosha.

Makamu wa Rais amesema kampeni ya uwekezaji katika sekta ya maji ilioyozinduliwa Jijini New York itasaidia kukusanya rasilimali zinazohitajika zaidi kwaajili ya utekelezaji wa programu ya uwekezaji katika sekta ya maji Barani Afrika. Amesema uwekezaji katika sekta ya maji utahitaji kuongezwa ili kufikia sehemu ya malengo ya maendeleo endelevu inayohusiana na maji safi na salama.

Mkutano huo umeongozwa na Mwenyekiti Mwenza wa jopo la viongozi wa juu wa programu ya uwekezaji katika sekta ya maji barani Afrika Rais wa Senegal Macky Sally pamoja na Mwenyekiti Mwenza mbadala wa jopo hilo Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne wa Tanzania Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete. Kampeni hiyo imezinduliwa kwa lengo la kukusanya dola za marekani bilioni 30 ikiwa na kauli mbiu isemayo “Mind the gap – Invest in Water”

By Jamhuri