Mtibwa Sugar wameungana na Simba sc Kucheza Mashindano ya Kimataifa baada ya Jana kutangazwa rasmi kuwa mabingwa wa Kombe la Shirikisho baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Singida United katika mchezo wa fainali uliopigwa Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.

Katika mchezo huo ulioanza kwa kasi huku Singida wakiongoza kumiliki mpira kwa kipindi cha kwanza ulishuhudiwa nyavu za Singida United zikianzwa kutikishwa mnamo dakika ya 22 na Salum Kiwimbwa.

Mkuu wa Mkoa wa Arusha,Mrisho Gambo alipomkabidhi mfano wa hundi ya shilingi milioni 50, nahodha wa mabingwa wapya wa Kombe la Shirikisho la Azam Sports, Shaaban Nditi.

Bao la Kiwimbwa lilidumu kwa dakika 15 tu ambapo katika dakika ya 37 Mtibwa walijipatia bao la pili kupitia kwa Issa Rashid ‘Baba Ubaya’ aliyefunga kwa mpira wa kona ulioenda moja kwa moja langoni na kumuacha kipa Ally Mustafa wa Singida United akiwa hana la kufanya.

Wakati dakika 45 za kwanza zikielekea kumalizika huku ubao wa matokeo ukisomea ni 2-1, Singida walipata nafasi ya kuandika bao la kwanza likitiwa kimiani na Chuku kwenye dakika ya 43, mpaka Mwamuzi anapuliza kipyenga kuashiria mapumziko, matokeo yalikuwa ni 2-1.

Kipindi cha pili kilianza tena kwa kasi huku Singida wakilishambulia zaidi lango la Mtibwa Sugar, na katika dakika ya 71 ya mchezo, mshambuliaji wa timu hiyo Tafadzwa Kutinyu aliisawazishia na kubadilisha ubao wa matokeo kwa kusomeka 2-2.

Kipindi hicho wakati mpira ukielekea mwishoni, kikosi cha Mtibwa kilibaki pungufu baada ya Baba Ubaya kutolewa nje kwa kadi ya nyekundu kufuatia mchezo usio wa kiungwana.

Kuondoka kwa Baba Ubaya hakukuwakatisha tamaa Mtibwa kwani walijitahidi kupigana na katika dakika ya 90, Ismail Kahesa aliweza kuiandikia timu yake bao la 3 na mpaka mchezo unamalizika, Mtibwa walikuwa mbele kwa mabao hayo matatu dhidi ya mawili ya Singida United.

Mtibwa sasa itakuwa mwakilishi wa michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa msimu ujao kufuatia kuchukua ubingwa huo, na hii ni kwa mujibu wa sheria na kanuni za TFF kuwa bingwa wa FA ataiwakilisha Tanzania katika mashindano hayo.

By Jamhuri