Hospitali ya Taifa Muhimbili imeahidi kushirikiana na nchi ya Namibia katika kujenga uwezo wa utoaji huduma za kibingwa na bobezi kwa wataalamu wa afya nchini humo.

Hayo yamesemwa leo na Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Prof. Mohamed Janabi wakati akiongea na Kamati ya Kudumu ya Bunge la Namibia ya Usawa wa Jinsia, Maendeleo ya Jamii na Mambo ya Familia ambayo ipo nchini kwa ziara ya kikazi ya kujifunza namna sekta ya afya inavyofanya kazi.

Prof. Janabi amesema kuwa katika kutekeleza jambo hilo Muhimbili inaweza kutuma wataalamu wa kada mbalimbali (pair) kwenda nchini humo kufanya kazi na wataalamu wao hatimaye kuwajengea uwezo au watalaamu hao kuja na wagonjwa wao kupata huduma za kibingwa nchini ili wajifunze kutokana na mazingira wezeshi yaliyopo.

“Sekta ya Afya nchini Tanzania imeendelea kukua siku hadi siku kutokana na uwekezaji unaofanywa na Serikali kwenye eneo la miundombinu, vifaa tiba na kusomesha wataalamu kwenye ngazi ya ubingwa na ubobezi katika nchi mbalimbali duniani ambao mara baada ya masomo yao, hurejea nchini kuwatumika Watanzania” amebainisha Prof. Janabi.

“Majanga ya magonjwa mlipuko hayawezi kuisha duniani, ambapo hivi karibuni tulishuhudia nchi zikifunga mipaka yake kutokana na mlipuko wa UVIKO-19, hivyo ni vizuri nchi zetu za Afrika kuwa na sekta ya afya imara ili kuwasaidia watu wake wakati wote na inapotokea changamoto yeyote”, amesema Prof. Janabi.”

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge la Namibia ya Usawa wa Jinsia, Maendeleo ya Jamii na Mambo ya Familia, Mh. Gotthard Kasuto amesema lengo la ziara yao nchini ilikuwa ni kujifunza kwani Tanzania imepiga hatua kubwa kwenye sekta ya afya.

Amesema kwamba kamati yake imetembelea Hospitali ya Benjamini Mkapa Dodoma, Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete, Taasisi ya Mifupa Muhimbili na Hatimaye Hospitali ya Taifa Muhimbili ambapo wamejionea uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali ya Tanzania kwenye vifaa tiba vya kisasa, uwepo wa watalaamu wazalendo wanaotoa huduma za kibingwa kwa watu wao.

“Itoshe kusema tumejifunza sana namna sekta ya afya Tanzania inavyofanya kazi, tumefurahia mazingira ya Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa kuwa ni masafi lakini zaidi ameona vifaa tiba vya kisasa ambavyo mara nyingi tumezoea kuviona katika nchi za magharibi” amesema Mhe. Kasuto.

Kwa upande wake mjumbe wa kamati hiyo Mh. Maria Kamutali amesema amefurahia namna ambavyo wataalamu wazawa ndio madaktari bingwa na wabobezi katika Hospitali walizotembelea tofauti na Namibia ambapo madaktari wengi ni wageni, hivyo ameahidi atakaporejea kwao atashawishi Serikali kuweka mazingira wezeshi kwa watoto kupenda masomo ya sayansi ili baadae waweze kuzalisha wataalamu wa afya wengi na wazawa.

Please follow and like us:
Pin Share