Watendaji wa Serikali wametakiwa kutoa fursa kwa wamiliki wa ardhi kunufaika na maeneo wanayomiliki pindi wawekezaji wanapohitaji ardhi kwa ajili ya uwekezaji.

Hayo yameelezwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Mwigulu Nchemba leo Juni 16, 2023 bungeni wakati akiwasilisha bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha wa 2023/24.

Mwigulu amesema kuwa maono ya Rais Samia Suluhu Hassan ni kuimarisha ushiriki wa sekta binafsi hivyo ni lazima watendaji wote serikalini wawe na nidhamu ya kuilea na kuiwezesha sekta binafsi kukua na kushiriki kikamilifu katika kukuza uchumi badala ya kufanya urasimu na kuwadhibiti.

“Tunatumia nguvu kubwa kwenye kudhibiti kuliko nguvu tunayoitumia kuwezesha.Lazima tuheshimu sekta binafsi na kutambua mchango wake katika kutoa ajira, kuondoa umaskini na kukuza uchumi. Nitoe rai kwa Watanzania wenzangu tuwe na nidhamu katika kuiwezesha sekta binafsi kukua.

“Hali ilivyo sasa, wawekezaji wa ndani wakijaribu kupiga hatua wanapigwa vita na kukatishwa tamaa. Hata wamiliki wa ardhi hawapati fidia stahiki pale wawekezaji wanapohitaji kumilikishwa ardhi hizo kana kwamba watanzania hawatakiwi kutajirika. Nitoe rai kwa watendaji wa Serikali, acheni Watanzania walipwe pesa nyingi, acheni Watanzania watajirike”amesema.