Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar ea Salaam

Mtoto mwenye umri wa miaka mitano, mkazi wa Jijini Dar es Salaam, mwishoni mwa wiki ametolewa pini kwenye mapafu yake kwa kutumia kifaa maalum chenye kamera kilichopelekwa moja kwa moja hadi ilipo, kuinasa na kisha kuitoa ambayo amekaa nayo kwa takribani mwezi mmoja.

Wazazi wa mtoto huyo (majina yamehifadhiwa) wanasema mtoto wao alianza kupata kikohozi na homa za mara kwa mara ndipo walipompeleka Hospitali kubwa ya binafsi jijini hapa ambapo walimfanyia baadhi ya vipimo vilivyoonesha uwepo wa maambukizi kifuani…akalazwa, kesho yake kufanyiwa kipimo cha X-Ray na kugundua uwepo wa pini ya kubandikia matangazo ambayo walijaribu kuitoa bila mafanikio na kuwashauri wazazi hao kumpeleka ama Kenya au Afrika ya Kusini ili kutolewa pini hiyo.

“Kabla ya kufikia uamzi wa kumpeleka Kenya au Afrika ya Kusini, mume wangu alisema aliona “clip” kwenye vyombo vya habari kuwa Hospitali ya Taifa Muhimbili hivi karibuni ilifanikiwa kumtoa mtoto Skrubu (Screw)…hivyo waliomba wapewe Rufaa kuja Muhimbili ambayo tulipewa na kupokelewa vizuri hapo Emergency ya Muhimbili ambao walimfanyia X-Ray na kuona pini ilipokaa na kutuambia kuwa mtoto wanamlaza na atafanyiwa procedure ya endoscope kesho yake,” amesema mama wa mtoto.

Ameeleza kuwa huduma hiyo ya kumtoa pini ilifanyika vizuri na kwa mafanikio makubwa ambapo mtoto hakohohi tena kama zamani na ni mwenye furaha.

“Huduma zinazotolewa Hospitali ya Taifa Muhimbili ni sawasawa na zile tunazofuata katika hospitali kadhaa kwani kuna watoa huduma wenye weledi, vifaa tiba vya kisasa, mahali pazuri pa kulala, huduma kwa wateja (customer care) ni nzuri, “ amesema mama huyo.

By Jamhuri