Mapema mwezi huu nikiwa Dar es Salaam nilituma ujumbe kuomba huduma ya usafiri wa Uber, huduma nafuu ya usafiri wa taksi ambayo imeleta nafuu ya gharama za usafiri jijini humo.

Katika kutumia Uber nimegundua tatizo moja la msingi. Madereva hawana uzoefu wa kutosha wa kusoma ramani kubaini mteja yuko wapi. Kwa sababu hiyo, wanalazimika kupiga simu au kutuma ujumbe mfupi wa maandishi kuuliza maswali ambayo yanajibika kirahisi kwa kufahamu vyema kusoma ramani.

Katika kujibu mojawapo ya maswali ya dereva aliyekuwa jirani na mimi, lakini bila kutambua wapi anipitie, niliandika ujumbe kusema kuwa nipo kwenye njia panda ya kuingia nyumbani kwa Mwalimu Nyerere. Yaliyotokea yaliniacha kinywa wazi kwa mshangao.

Lile gari lilinipita likielekea upande tofauti na nilipokuwa, na baada ya muda kidogo, na kutokana na maelekezo yangu, alifika nilipokuwa na alinichukua.

Niliamini lilikuwa gari ambalo lilitoa huduma kwenye maeneo ya jirani na nilipokuwa, kwa hiyo swali langu la kwanza kumuuliza lilikuwa: “Hupafahamu nyumbani kwa Mwalimu Nyerere?”

Dereva wa taksi? Dar es Salaam? Hufahamu nyumbani kwa Mwalimu Nyerere? Na wala hujawahi kusikia kituo “Kwa Mwalimu Nyerere”?

Alisema kuwa amewahi kusikia kituo cha Mwalimu Nyerere, lakini hakufahamu kuwa ndiyo pale aliponichukua. Alisema yeye anaishi Mbagala kwa hiyo hafahamu vyema maeneo ya Mikocheni. Dar ni jiji kubwa, aliniambia. Kwa kuongezea, aliniambia kuwa yeye ni mwenyeji wa Wilaya ya Rorya, mojawapo ya wilaya za mkoa wa Mara, wilaya inayopakana na Kenya.

Nilimwambia hawezi kuwa anatokea Rorya, labda aniambie kwao Kisumu, mji uliyopo kwenye jimbo la Nyanza nchini Kenya, linalopakana na Wilaya ya Rorya. Alisema nimuombe radhi, ama sivyo tungefikishana polisi.

Mazungumzo yote yalikuwa ya utani kwa hiyo isingefikia hali ya kufikishana polisi, lakini nilisisitiza kwake kuwa Uber wanahitaji kuongeza ujuzi wa madereva wake kufahamu vyema maeneo ambayo wanahudumia, pamoja na kuwapa mafunzo bora ya kusoma ramani.

Tukiendelea na safari nilipokea simu na kutokana na maudhui ya mazungumzo yangu kwenye simu yule dereva akahisi upo uhusiano kati yangu na familia ya Mwalimu Nyerere. Akaniambia: “Sasa naelewa kwa nini ulikasirika.”

Nilimwambia sikukasirika. Nilishangaa tu, kwamba yupo dereva wa taksi Dar es Salaam ambaye hafahamu nyumbani kwa Mwalimu Nyerere. “Na ndiyo maana,” nikasisitiza, “nahisi kwenu ni Kisumu.”

Nilikumbuka haraka kuwa hata kama Mwalimu Nyerere mwenyewe angeshangaa kama mimi kutofahamika anapoishi, angekuwa mtu wa kwanza kuhoji sababu ya Waafrika kuanza kuulizana maswali juu ya uraia wao.

Malengo ya Jumuiya ya Afrika Mashariki aliyoiasisi na Mzee Jomo Kenyatta, na Dk. Milton Obote bado yanaongoza nchi wanachama wa Afrika Mashariki kuelekea kwenye hali ambayo itaruhusu raia wa nchi moja kuwa huru kutafuta ajira kwenye nchi yoyote mwanachama bila kuhitaji vibali vya kazi, kama ilivyo sasa.

Ni sehemu tu ya mlolongo wa malengo yenye nia ya kuimarisha ushirikiano katika nyanja za siasa, uchumi, jamii na sanaa, utafiti na teknolojia, ulinzi, usalama, sheria na katiba.

Pamoja na kuwa lengo la awali ilikuwa ni kufikia uundwaji wa shirikisho la kisiasa, lengo hili sasa limebadilishwa na kuwa lengo la kuunda aina ya shirikisho ambalo linapunguza mamlaka na nguvu ya serikali moja ya shirikisho na kubakiza hayo mamlaka kwenye serikali za nchi wanachama.

Hali hii siyo kusudio la viongozi kama Kwame Nkrumah wa Ghana, na Mwalimu Nyerere na viongozi wengi wa Bara la Afrika na wenye asili ya Afrika ambao waliamini kuwa silaha kubwa ya Waafrika na watu wa asili ya Afrika itakayolinda maslahi yao na kuwaletea maendeleo ya kweli ni umoja wa kweli, wa kisiasa na kiuchumi, wa serikali moja.

Hawa ndiyo walikuwa viongozi ambao hawakupendelea kumuuliza mkazi wa Kisumu anafanya nini Dar es Salaam akilazimisha kuendesha taksi ya Uber bila kuyafahamu maeneo muhimu ya jiji, ila waliendelea kuhoji na kuweka mikakati yenye malengo ambayo yangempa nafasi Mwafrika yeyote kusafiri, kuishi, na kufanya kazi kwa uhuru kwenye nchi yoyote iliyopo kati ya Cairo na Cape Town.

Baada ya kumsema, ikawa ni hoja niliyomrushia rafiki yangu wa Kisumu, kwa njia ya Rorya. Nilianza kuhoji ni zipi sababu za msingi ambazo zinaweza kutolewa kutetea hoja inayomzuia mtu anayefuata taratibu zilizopo za kisheria kuja Tanzania na kuanzisha shughuli yoyote ya kiuchumi ambayo itamlazimu kutumia huduma mbalimbali, kununua bidhaa, kuajiri wafanyakazi, na kulipa kodi.

Na kumzuia kufanya hivyo kwenye mazingira ambayo siyo kila Mtanzania mwenye uwezo wa kutimiza hayo. Swali ambalo sikuuliza ni: “Ni bora serikali ikusanye kodi kwa raia wa Kenya anayefanya kazi Tanzania, au ikose mapato kwa sababu raia wa Tanzania bado hana uwezo wa kulipa kodi?”

Yote hayo yakifanyika katika malengo yale makuu ya kuimarisha ushirikiano wa kikanda miongoni mwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Hakuniunga mkono kwa dhati wazo langu, labda kwa sababu hakuamini mtu huyo huyo aliyeanza kumshutumu anatokea Kisumu aanze tena kutetea hoja ya kuwapo raia wa nje wanaoweza kunufaisha uchumi wa Tanzania.

Sina hakika kama raia wa upande mmoja wa Jumuiya wataunga mkono malengo ya Jumuiya iwapo wataanza kupokonywa ajira na raia wa upande mwingine wa Jumuiya pamoja na kuendeleza ushirikiano uliyopo kati ya nchi wanachama utaendelea kuimarika.

Hata hivyo, naamini zipo faida za msingi zaidi za uimarishwaji wa uchumi, ukuaji wa mapato, na ushawishi mkubwa zaidi wa kisiasa katika masuala ya kimataifa kwa Jumuiya zaidi kuliko kwa nchi moja moja.

Inahitajika mikakati ya kuelimisha umma kutambua faida za muda mrefu za ushirikiano, na mikakati mahususi kuhakikisha kuwa faida zitakazojitokeza haziwaachi raia wa nchi wanachama wakijuta na wakitamani kuunga mkono utengano badala ya umoja.

Nilimwongezea alama za ufaulu rafiki yangu wa Kisumu/Rorya baada ya kunijulisha kuwa anafahamu ilipo nyumba ya Mzee Ali Hassan Mwinyi.

Please follow and like us:
Pin Share