Na Mwamvua Mwinyi,JamhuriMedia,Pwani

Lasmini Kondo mwanafunzi wa kidato cha kwanza katika shule ya sekondari ya Masaki wilayani Kisarawe mkoani Pwani,amekutwa akiwa amejinyonga baada ya kukatazwa na wazazi wake kutojihusisha na mapenzi .

Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Pwani ,ACP Pius Lututumo amesema mwanafunzi huyo amejinyonga baada ya kugombezwa na wazazi wake kutojihusisha na mapenzi kufuatia kukutwa na barua aliyokua amemuandikia mpenzi wake.

“Baada ya wazazi wake kukuta barua ambayo marehemu alimuandikia mpenzi wake walimfokea kwa kumtaka kuachana na masuala hayo kwani yeye ni mwanafuzi.

“Kutokana na kitendo hicho marehemu aliamua kuchukua uamuzi wa kujinyonga jambo ambalo linasikitisha,” amesema.

Katika tukio lingine,Kamanda Lutumo ameeleza kuwa Pili Mang’ota ambae ni mkulima wa mboga mboga na mkazi wa Sanze Kisarawe ,amekutwa amefariki dunia.

“Mwanamke huyu aliaga kwenda Visegese kuchukua mboga lakini hakurudi tena hadi umauti ulipomkuta na kukutwa vichakani akiwa amefukiwa akiwa amefariki”alifafanua Lutumo.

Kufuatia kifo cha mwanamke huyo, jeshi hilo linamsaka mtu mmoja aliyejulikana kwa jina la Abdallah ambae ni mume wa marehemu kwa tuhuma za kuhusika na kifo cha mkewe .