Watu watano wameripotiwa kufariki dunia papo hapo, katika eneo la Mikumi, wilayani Kilosa mkoani Morogoro kwenye ajali iliyohusisha gari ndogo maarufu kama IT iliyokuwa ikitokea bandarini jijini Dar es salaam kuelekea mpakani Tunduma kugongana uso kwa uso na gari kubwa la kusafirisha mafuta  lilokuwa likitokea mkoani  Iringa kuelekea mkoani Morogoro.

Kamanda wa jeshi la polisi mkoani Morogoro Fortunatus Musilimu amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo kuwa ajali hiyo imetokea majira ya usiku wa kuamkia jumatatu eneo la Iyovi wilayani Kilosa barabara kuu ya Morogoro – Iringa na kubainisha chanzo cha ajali hiyo kuwa ni uzembe wa dereva aliyekuwa akiendesha gari ndogo aliyefahamika kwa jina la Festo Shoo ambaye alikuwa katika mwendo kasi na kutaka kuyapita magari yaliyokuwa mbele yake bila kuangalia kwa makini mbele yake.

Kamanda Musilimu amesema waliopoteza maisha katika ajali hiyo kuwa ni watu watano wanaume wanne na mwanamke mmoja ambao wote walikuwa katika gari dogo (IT).