Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia, Kilimanjaro

Mwanafunzi wa kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari St.Mary Goreti iliyopo Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro Robert Meier (17), amejiua kwa kujipiga risasi na kuacha ujumbe mwili wake uchomwe.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa akizungumza na waandishi wa habari leo amethibitisha kutokea kwa tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia juzi mkoani Kilimanjaro.

Kamanda Maigwa amesema kuwa siku ya tukio saa 8, usiku wa kuamkia juzi huko Mwereni katika Kata ya Ngangamfumuni, mwanafunzi huyo alijiua kwa kujipiga risasi kifuani upande wa kushoto kwenye moyo na risasi hiyo ikatokea mgongoni.

Kamanda amesema kuwa kabla ya mwanafunzi huyo kujiua, aliacha ujumbe wa maandishi ulisomeka mwili wake uchomwe na majivu yake yasafirishwe kwenda Marekani yakazikwe pembezoni mwa kaburi la baba yake ambaye alizikwa nchini humo.

Amesema mwanafunzi huyo alijiua kwa kwa kutumia bastola yenye namba LXE 023 aina ya Glock iliyotengenezwa nchini Austria, inayomilikiwa kihalali na mtu aitwaye Boniface Kimario, mkazi wa Mwereni.

Kamanda amesema kuwa Jeshi la Polisi linamshikilia mmiliki wa bastola hiyo kwa mahojiano zaidi na kuwataka wamiliki wa silaha wanaozimiliki kihalali kuwa makini na utunzaji wa silaha hizo ili kuepusha madhara yanayoweza kujitokeza.

By Jamhuri