Mwanamke aliyenusurika kifo kisa dini

Meriam Yahia Ibrahim Ishag au Maryam Yahya Ibrahim Ishaq ni raia wa Sudani kwa anayeishi nchini Marekani katika Jimbo la Philadelphia kwa sasa, kutokana na kukimbia nchini kwake baada ya kupona hukumu ya kifo kwa madai ya kuasi dini yake.
Alizaliwa Novemba 3, 1987 katika mji wa Al Qadarif na kuwa mwanamke wa kwanza kuhukumiwa kifo kwa madai ya kuuasi Uislamu na kuingia katika Ukristu. Alikamatwa akiwa na ujauzito na kufungwa katika gerezani Mei 27, 2014.
Kifungo hicho kinaelezwa kuwa ni mfululizo wa mateso wanayoyapata Wakristu nchini Sudan. Baba yake Meriam Ibrahim alikuwa Mwislamu baadaye, lakini yeye alilelewa katika mazingira ya Kikristu. Aliolewa mwanaume wa Kikristu, Daniel Wani.
Kutoka na hatua hiyo, Meriam ilishtakiwa katika Mahakama ya Sudani kwa madai ya kwamba alikuwa anafanya uzinzi kutokana na kuolewa na mwanaume asiyekuwa Mwislamu.
Kushtakiwa kwa Meriam kunatokana na kaka yake wa kambo, Al Samani Al Hadi Mohamed Abdullah, alimfungulia mashtaka dada yake wakitaka ahukumiwe kwa kwa kosa la kuasi dini.
Hata hivyo, mume wake kwa kushirikiana na mawakili waliomtetea, walisema kwamba hatua ya ndugu hao kufungua mashtaka  hayo ni kwamba walitaka kufanya hivyo ili wamiliki biashara za Meriam baada ya kuona amepata mafanikio makubwa kwa muda mfupi.
Meriam alikuwa anamiliki saluni ya kutengeneza nywele, duka na ardhi kwa ajili ya kilimo.
Alihukumiwa kifo Mei 15,  2014 kwa madai ya kufanya uasi kutoka kwenye Uislamu. Alishtakiwa kwa kosa la kubadili dini kutoka kwenye Uislamu kwenda katika Ukristu.
Lakini siku zote Meriam amekuwa akisisitiza kuwa yeye ni Mkristu, na hata katika utetezi wake, Meriam alidai kwamba siku zote na wakati wote amekuwa akifuata imani ya mama yake.
Meriam alikataa ushauri ulitolewa na hakimu uliomtaka kujifikiria upya na kuukana Ukristu, bali alisisitiza kuwa yeye si Mwislamu bali ni Mkristu.
Alipewa siku tatu za kufanya hivyo lakini aliporudishwa tena kizimbani, bado aliendelea na msimamo wake wa kukataa kubadili dini yake na kusisitiza kwamba yeye ni Mkristu na amelelewa katika mazingira hayo katika maisha yake yote, hivyo hayuko tayari kuukana.
Hakuwa tayari kubadili imani yake pamoja na kuwapo kwa ombi la mahakama.
Alihukumiwa kunyongwa lakini mume wake, Daniel Wani, alipigania haki yake, hivyo alikata rufaa dhidi ya hukumu zote mbili na kushinda.
Juni 24, 2014 Meriam aliachiwa kwa amri ya Mahakama ya Rufaa ya Sudan. Lakini siku iliyofuata alikamatwa tena yeye na familia yake akiwa safarini kwenda Marekani. Alipelekwa mjini Khartoum kwa ajili ya mahojiano na Polisi  wa Sudan.
Balozi wa Marekani aliitwa katika mahojiano hayo baada kudaiwa kutoa visa iliyoelezwa na Serikali ya Sudan ukiukaji wa makosa ya jinai.
Meriam alikuwa huru tena Juni 26, 2014 na alikimbilia katika ubalozi wa Marekani nchini Sudan akiwa na familia yake. Baada ya majadiliano ya kina, hatimaye aliondoka Sudan na kwenda Roma, Julai 24, mwaka huu ambapo alikutana na Papa Francis.
Meriam alisafirishwa hadi nchini Italia baada ya kuwa kwenye ubalozi wa Marekani mjini Khartoum kwa zaidi ya mwezi mmoja. Yeye na familia yake waliondoka kwa ndege ya Serikali ya Italia wakiongozana na Waziri mmoja wa Italia, Lapo Pistelli.
Baada ya kuwasili Italia, Meriam alikutana na Papa Francis ambaye alimsifu kwa kusimamia dini ya Ukristo licha ya tishio la mauti.
Mwanamke huyo alikutana na Papa katika makao yake rasmi ya Santa Marta yaliyoko kwenye Makao Makuu ya Kanisa Katoliki ya Vatican.
Meriam alihukumiwa kunyongwa mapema mwaka huu lakini baadaye akaachiliwa huru mwezi Juni, baada ya ulimwengu mzima kukemea uamuzi huo uliotolewa na mahakama moja nchini humo. Lakini Meriam amesisitiza kuwa hajawahi kuwa muumini wa dini ya Kiislamu kwani alilelewa na mamake ambaye ni Mkristo.
Kutokana na malalamiko kutoka ulimwenguni kote, aliachiliwa huru mwezi Juni. Maya, bintiye yake Meriam, alizaliwa gerezani mwezi Mei.
Baada ya kuachiliwa kutoka gerezani, Meriam alizuiliwa kutoka nchini Sudan na familia yake ikalazimika kutafuta hifadhi katika ubalozi wa Marekani uliopo Khartoum.
Aliwasili Philadelphia kwa ndege Julai 31 jioni kutoka Rome, Italia akiwa na mume wake, Daniel Wani, ambaye ni raia wa Marekani. Wani, mzaliwa wa Sudan Kusini lakini mwenye uraia wa Marekani, ni muumini wa dini ya Kikristu.
Meriam alikaribishwa kwa namna ya kipekee alipopitia Philadephia na kutajwa kuwa ‘mpigania uhuru wa kimataifa’ na Mstahiki Meya wa  Philadelphia, Michael Nutter. Nutter pia alisema watu watakumbuka Meriam kama ‘wengine waliotupigania kuwa huru,’ na kumlinganisha Meriam na Rosa Parks.
Parks alisifika na kutazamwa kuwa ushujaa wa harakati za haki za kiraia nchini Marekani, alipokataa kuondoka katika kiti ndani ya gari ili ampishe mwanamume Mzungu huko Alabama.
Nutter alimkabidhi Meriam mfano wa ‘kengele ya uhuru,’ ambayo ni ishara ya uhuru wa Marekani.
Safari ya Meriam iliishia New Hampshire kwani alikuwa anasubiriwa kwa hamu na jamaa na wafuasi wake katika uwanja wa ndege. Alikaribishwa na halaiki ya watu, wengine huku wakiimbia “Marekani iishi milele.”
Mumewe alitoa hotuba fupi na kushukuru Serikali ya Marekani na Maseneta wa New Hampshire kwa kumpigania na kwa kufanya mipango ya kumpa mke wake hifadhi. Pia aliwashukuru watu wa Sudan kwa kuwasaidia.
Familia ya Meriam inakusudia kuishi New Hampshire iliko familia ya mume wake.
Sudan ni nchi inayofuata sharia ya dini ya Kiislamu, hivyo ni kosa kwa mwanaume wa mwanamke wa dini ya Kiislamu kuolewa na mtu asiyekuwa Mwislamu.
Sharia ya Kiislamu hairuhusu ndoa kati ya wanawake wa Kiislamu na wanaume ambao si Waislamu, hivyo ndoa ya Meriam Ibrahim ilihesabika kuwa ni batili pamoja kusajiliwa nchini humo.

Hali aliyokuwa nayo gerezani

Meriam alifungwa katika Gereza la Wanawake la Omdurman akiwa na mtoto wake, Martin Wani, mwenye umri wa miezi 20. Awali wageni hawakuruhusiwa kumuona, mara ya mwisho mumewe kumuona alikuta amefungwa pingu katika miguu yake na ilikuwa imevimba.
Pamoja na hali hiyo uongozi wa gereza hilo hawakuruhusu Meriam kwenda kutibiwa hospitali.  
Japo alikuwa na pingu miguuni lakini wakati wa kujifungua ilibidi afunguliwe pingu baada ya kuonekana kuna uwezekano wa mtoto wake kupata ulemavu wa kudumu.
Mohamed Jar Elnabi, mwanasheria anayemwakilisha Meriam, ndiye aliyewataka polisi na Mahakama kumruhusu mumewe kumtembea Meriam.
Katika kesi hiyo, Meriam iliwakilishwa na wanasheria watano: Elshareef Ali Mohamed, Mohamed Elnbi, Mohamed Mustaf, Osman Mobarak, Thaiut Alzaber.
Elshareef Ali Mohamed ni mwanasheria wa kimataifa mwenye elimu ya sheria ya kimataifa (LLM) katika kutetea haki za binadamu kutoka Chuo Kikuu cha Birmingham City.
Pia ni mjumbe wa Tume ya Afrika ya kutetea haki za binadamu, aliyeongoza kampeni ya kutetea haki za binadamu. Anafanya kazi Umoja wa Mataifa kama Afisa wa haki za binadamu. Yeye pia anafanya kazi na Shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu (Amnesty International-AI).