Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia

Mwanaume mmoja anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 30 mpaka 35 amekutwa amefariki katika bwawa dogo lililopo katika msitu wa Tanwat eneo la Kibena Mjini Njombe.

Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo ambao ni walinzi katika msitu ya Tanwat uliopo karibu na bwawa hilo wamesema kuwa mnamo majira ya saa 11;10 alfajiri ya tarehe 21,2022 waligundua uwepo wa mtu ambaye alikuwa akisogea katika bwawa hilo huku akiwa ameshika tochi na baada ya kufika akaanza kuingia ndani ya bwawa hilo na hata walipojaribu kumuita ili atoke nje ya bwawa hakuwasikiliza.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuutoa mwili katika bwawa Kaimu Kamanda wa Mkoa wa Njombe, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Inspekta Joel Mwakanyasa amethibitisha kutokea kwa tukio hilo.
Baada ya mwili huo kutolewa katika bwawa, Jeshi la Zimamoto liliwataka wananchi kuutambua mwili huo lakini hakuweza kufahamika mara moja .
Kufuatia tukio hilo Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoani Njombe limewaasa wananchi kuacha mara moja tabia ya kusogelea maji yenye kina kirefu ikiwa hawana uwezo wa kuogelea.