*Yanga safiii… ila Simba mmh!

DAR ES SALAAM

Na Andrew Peter

“Mwanza oooh Mwanzaaa! Mwanza mji mzuri. Mwanzaaaa!” Maneno ya Dk. Ramadhan Remmy Ongala ‘Mbele kwa Mbele’.

Hakuna anayebisha kuhusu uzuri wa Jiji la Mwanza maarufu kama ‘Rocky City’ kutokana na miamba na majabari yanayolipamba.

Jiji la Mwanza lipo pembezoni mwa Ziwa Victoria. Mawe yaliyopo katika eneo la Nyanza pamoja na jiwe maarufu

la Bismarck lililopo ndani ya ziwa eneo la Bustani ya Kamanga Feri ni kivutio tosha kwa mashabiki wa Yanga na Simba watakaokwenda kushuhudia nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC).

Uwanja wa CCM Kirumba una uwezo wa kuchukua mashabiki 35,000, hakuna shaka kwamba uwanja huo utajaa kutokana na Jiji la Mwanza kuwa na wakazi wanaokadiriwa kufikia 426,154; mkoa mzima ukiwa na watu zaidi ya milioni 3.2, kwa mujibu wa takwimu za NBS zilizochapishwa kwenye tovuti ya Halmashauri ya Jiji www.mwanzacc.go.tz; idadi inayoweza kuongezeka zaidi baada ya Sensa ya Watu na Makazi ya Agosti 23, 2022.

Mwanza ni mmoja ya mikoa yenye wakazi wenye uchumi mzuri kutokana na shughuli zao mbalimbali kiasi cha kuifanya halmashauri ya jiji hadi nusu ya mwaka huu kukusanya zaidi ya Sh bilioni 11; makusanyo ya mwaka wa fedha 2021/22, hivyo uwepo wa mchezo wa watani wa jadi ni neema nyingine kwa jiji hilo.

Pamoja na uzuri wote huo, mabingwa watetezi wa Kombe la ASFC, Simba wanashuka Rocky City wakiwa na

rekodi ya kushinda mechi moja tu kati ya sita za mashindano ilizocheza dhidi ya Yanga mkoani Mwanza tangu mwaka 1974.

Simba watakuwa wageni wa Yanga katika mchezo wa nusu fainali ya kwanza ya Kombe la ASFC itakayochezwa

Mei 28, kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, nusu fainali ya pili itakuwa Mei 29, ikiwakutanisha Azam dhidi ya Coastal Union kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.

Vijana wa Pablo Martin watashuka Kirumba wakiwa na lengo moja tu; kusaka ushindi ili kujihakikishia kufuzu

kwa fainali na kujiweka katika mazingira ya kutetea taji msimu huu baada ya kupoteza mwelekeo katika Ligi Kuu.

Hata hivyo, rekodi zinaonyesha Mkoa wa Mwanza si sehemu salama kwa Simba kwani tangu mwaka 1974 wamefanikiwa kushinda mechi moja tu, 2-0, mwaka 2005, mabao ya Emmanuel Gabriel na Mussa Hassan ‘Mgosi’, ikipata sare moja ya 1-1 mwaka 2001.

Wenyeji Yanga wameshinda mechi nne walizocheza dhidi ya Simba mkoani Mwanza, ukianza ile ya kwanza ya

mwaka 1974 iliyochezwa Uwanja wa Nyamagana. Katika mchezo huo mabao ya Yanga yalifungwa na Gibson

Sembuli na Sunday Manara, bao la kufutia machozi la Simba likifungwa na Adam Sabu.

Yanga wanakwenda katika mchezo huo kwa lengo la kulipa kisasi. Kwanza cha kunyukwa mabao 4-1 katika

nusu fainali ya 2019/20, kabla ya kufungwa 1-0 fainali iliyopita.

Mbali ya kisasi, Yanga wanataka kuandika rekodi nyingine ya kutwaa mataji yote mawili kwa mara ya pili ndani ya

msimu mmoja kama walivyofanya Simba misimu miwili iliyopita.

Kocha wa Yanga, Nabi, atakuwapo katika mchezo huu baada ya kuukosa ule wa ligi kutokana na adhabu, jambo

linalorudisha faraja kwa mashabiki wa Jangwani.

Katika mechi mbili za ligi, Yanga na Simba wameshindwa kufungana kutokana na mbinu za kiuchezaji na uchezaji

unaofanana kwa sasa kwani makocha wao hutumia mfumo mmoja; 4-2-3-1, jambo linalofanya mpira kuchezwa muda mwingi katikati ya uwanja na mashambulizi ya kushtukiza.

Hakuna shaka Nabi na Martin watakuwa wamewaandaa vema vijana wao kuelekea kwenye penalti iwapo mshindi

hatapatikana katika dakika 120 za kawaida.

Azam v Coastal Union vita ya heshima

Mabingwa wa 2018-19 wa Kombe la ASFC, Azam, watakuwa na kibarua kizito mbele ya Coastal Union katika mchezo utakaochezwa Mei 29, kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, jijini Arusha.

Jahazi la Azam msimu huu linakwenda mlama katika Ligi Kuu ikiwa nafasi ya tano, matumaini yao pekee ya kupata tiketi ya kucheza mashindano ya kimataifa ni kuhakikisha wanafuzu kwa fainali na hatimaye kunyakua ubingwa huo.

Coastal Union wenyewe pamoja na kufuzu kwa nusu fainali hii bado wapo kwenye janga la kupambana kuhakikisha hawashuki daraja msimu huu.

Jambo linalofanya nusu fainali hii kuwa na mvuto wa aina yake, hasa kutokana na nafasi ya timu hizo katika ligi. Pia mechi baina yao kuwa na ushindani mkubwa.

Hata hivyo, mabingwa wa Ligi Kuu 1988, Coastal Union hali yao ya uchumi si nzuri kwa sasa, hivyo kufuzu kwao

kwa fainali kutawapatia fedha za kutosha za kujenga kikosi chao kwa msimu ujao.

Matokeo ya Mwanza: Yanga v Simba

AGOSTI 10, 1974: Yanga 2-1 Simba

JUNI 30, 1996: Yanga 2-0 Simba (Hedex Cup)

SEPTEMBA 30, 2001: Simba 1-1 Yanga

APRILI 20, 2003: Yanga 3-0 Simba

JULAI 2, 2005: Simba 2-0 Yanga

OKTOBA 16, 2010: Yanga 1-0 Simba

MEI 28, 2022: Yanga Vs Simba

By Jamhuri