WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amesisitiza Wakuu wa Nchi na Serikali Zisizofungamana na Upande Wowote (NAM) wahakikishe wanashiriki katika kila tukio la umoja huo pamoja na kuendeleza ushirikiano katika masuala ya ulinzi na usalama pamoja na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Ameyasema hayo jana Ijumaa, Januari 19, 2024 wakati akihutubia katika Mkutano wa 19 wa Wakuu wa Nchi na Serikali zisizofungamana na Upande wowote (NAM) ulioanza tarehe 15 – 20 Januari, 2024. Waziri Mkuu anamwakilisha Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika mkutano huo.

“Tumezungumzia hali ya mabadiliko ya tabia nchi na namna tunavyopata athari kwenye maeneo yetu na umuhimu wa kuweka mkakati wa namna ya kudhibiti mabadiliko ya tabia ya nchi kwenye maeneo yetu.”

Masuala mengine ambayo Mheshimiwa Majaliwa aliyawekea msisitizo katika mkutano huo ni pamoja na kutoa wito kwa mashirika ya Umoja wa Mataifa kuangalia ajenda za NAM na kuona namna ya kushirikiana na NAM katika kuzitekeleza.

Mkutano huo wa siku mbili ulianza jana Ijumaa, Januari 19, 2024 katika Kituo cha Mikutano cha Ruwenzori, Speke Resort Kampala nchini Uganda. Katika mkutano huo Rais wa Uganda alikabidhiwa rasmi uenyekiti wa kundi hilo.

Mkutano wa NAM hufanyika kila baada ya miaka mitatu na Mkutano wa mwisho, wa 18 ulifanyika jijini Baku nchini Azerbaljan mwezi Oktoba, 2019. Mkutano huo haukuweza kufanyika tangu mwaka 2019 kutokana na janga la ugonjwa wa COVID-19 lililoikumba dunia.

Mkutano huo unalenga kuimarisha ushirikiano kwenye masuala ya biashara, uwekezaji, kutokomeza umaskini, mabadiliko ya tabianchi, amani na usalama katika mipaka, sekta ya afya, mandeleo endelevu, na uchumi wa kidijiti.

Umoja huo ulianzishwa wakati wa enzi za vita baridi ili kusaidia nchi wanachama wake kutoka mabara ya Asia, Afrika na Latin Amerika kuondokana na ukoloni ili kuweza kujitawala kisiasa, kiuchumi na kijamii.

Mapema jana Januari 19, 2024, Mheshimiwa Majaliwa alikutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Sri Lanka Mheshimiwa Ranil Wickremesinghe ambapo pamoja na mambo mengine wamejadiliana kuhusu kuimarisha uhusiano baina ya nchi hizo mbili ikiwemo uwekezaji kwenye sekta ya madini na biashara.

“Bado Taifa limeendelea na kauli mbiu yetu ya kuboresha diplomasia ya uchumi na tumewakaribisha Sri Lanka kuja kuwekeza kwenye sekta ya madini, viwanda na kilimo. Sri Lanka ni wanunuzi waziri wa madini ya vito, kahawa, chai, korosho na mazao ya mbogamboga.”

Naye, Sri Lanka Mheshimiwa Ranil Wickremesinghe alisema nchi yake ipo tayari kuwekeza nchini na amemuhakikishia Waziri Mkuu kwamba wapo tayari kufungua ubalozi nchini Tanzania ili kuimarisha ushirikiano wa kidiplomasia na kurahisisha shughuli za uwekezaji na biashara.

Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje Na Ushirikiano wa Afrika Mashariki January Makamba alisema miongoni mwa mambo yaliyojadiliwa na viongozi hao ni pamoja na urahisi wa wananchi wa Sri Lanka kutembelea Tanzania na Watanzania kutembelea Sri Lanka, hivyo masuala ya mabadiliko ya mfuko wa visa ili kuweza kurahisisha zoezi hilo.

“Mkutano huu umefungua fursa ya kuanzishwa kwa tume ya pamoja ya mashirikiano, Mheshimiwa Waziri Mkuu na Rais wa Sri Lanka wametuelekeza sisi Mawaziri wa Mambo ya Nje tukae na kutengenezwa tume hiyo kwa ajili ya kuratibu mashirikiano baina ya nchi zote mbili.”

Pia, Waziri Makamba alisema miongoni mwa mafanikio ya mkutano huo ni pamoja na nchi hiyo kukubali kufungua ofisi ya ubalozi nchini, ikiwa ni jitihada za kuongeza uwakilishi katika nchi za Afrika.

Alisema Tanzania na Sri Lanka ni wanachama wa umoja wa nchi zilizo katika Bahari ya Hindi na Sri Lanka kwa sasa ndiye mwenyekiti na sasa kuna masuala yanazungumzwa ikiwemo hifadhi ya mazingira ya bahari hiyo, usafiishaji na usalama na Tanzania imeahidi kuipa ushirikiano ili kuhakikisha malengo ya umoja huo yanatimia.

By Jamhuri