Na Wilson Malima, Jamhuri Media.

Waziri wa Habari Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Moses Nnauye amesema, licha ya kuongezeka kwa matumizi ya TEHAMA  duniani, ushiriki wa Wanawake na Wasichana bado upo Chini hasa katika nchi zinazoendelea.

Amesema, nchini  Tanzania bado kuna pengo kubwa la kidijitali kati ya wanawake na wanaume.

Waziri Nape ameeleza hayo  leo Machi 07  katika kongamano la Wanawake na Teknolojia liliandaliwa na Taasisi ya Launch Pad Tanzania lililofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa JNICC jijini Dar es Salaam.

“Licha ya kuongezeka kwa matumizi ya ICT kwa nchi nyingi  duniani, ushiriki wa Wanawake na Wasichana bado ni wa mdogo sana, hasa katika nchi zinazoendelea, kama ilivyo kwa Tanzania. Katika nchi yetu Sekta ya teknolojia bado ina pengo kubwa la kijinsia hususani kwa wanawake walio chini ya majukumu ya uongozi na nguvu kazi.”amesema Waziri Nape

Nape amesema Sekta ya teknolojia bado ina pengo kubwa kijinsia licha ya idadi ya wanawake kuwa kubwa takribani asilimia 51 kati ya Watanzania Milioni 61 kulingana na takwimu za Sensa ya mwaka 2022.

Naye Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia nchini, Nathani Belete amebainisha kuwa bado kuna changamoto kubwa zinazomzuia mtoto wa kike katika maendeleo ya kidijitali na teknolojia.

Amesisitiza kuongezewa uwezo na uelewa wa kidijitali kwa Watoto wa kike lakini pia kuhakikisha uwepo wa miundombinu ya kidijitali na Teknolojia kwa wanawake na wasichana wote wa mjini na vijijini.

By Jamhuri