Na Cresensia Kapinga, JamhuriMedia, Songea.

Waziri wa nchi ofisi ya Waziri Mkuu Kazi,Ajira, Vijana na wenye Ulemavu,Profesa Joyce Ndalichako, ameyaagiza mashirika ya Hifadhi za Jamii hapa nchini kuchukuwa hatua za haraka ili kutatua kero zinazowakabili wastaafu ikiwemo kucheleweshewa mafao yao baada ya kustaafu.

Maagizo hayo ameyatoa leo wakati akizindua mpango wakushughulikia kero za wastaafu uliozinduliwa katika viwanja vya ofisi ya Hazina ndogo iliyopo Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, ambapo alisema kuwa mwaka 2019 serikali ilikuwa inadaiwa na wastaafu zaidi ya kiasi cha sh. Trioni 2 lakini hadi kufikia mwaka huu wameweza kulipa wastaafu kiasi cha sh. Trioni 2.17 na kwamba wizara inaendelea kuwalipa wastaafu.

Waziri wa nchi ofisi ya Waziri Mkuu Kazi Ajira Vijana na wenye Ulemavu Profesa Joyce Ndalichako akizindua kitabu cha kumbukumbu za watumishi wa shirika la Mfuko wa Hifadhi ya Jamii, PSSSF.

Profesa Ndalichako amesema kuwa kisheria mstaafu anatakiwa kulipwa fedha ya kustaafu kutokana mshahara wake wa mwisho kutoka ambapo mwajiri anatakiwa kupeleka mchango mwezi mmoja baada ya mshahara wake kutoka.

Amefafanua zaidi kuwa wizara yake inatekeleza wajibu bila kusababisha kero licha ya kuwa wamekuwa wakipokea changamoto mbalimbali za wastaafu ambapo serikali imekuwa ikioneaha nia ya kuwasaidia wastaafu na kwamba mfuko ulikuwa na changamoto kubwa za madeni ambayo yalikuwa hayajalipwa.

Profesa Ndalichako amesema kuwa Desemba 2021 serikali ilikuwa tayari imeshalipa kiasi cha sh. Trioni 2.17 ambapo kabla yake mfuko wa Pensheni (PSSSf) ilikuwa inadaiwa na wastaafu kiasi kikubwa cha fedha.

“Ndugu zangu Serikali inayatambua matatizo ya wastaafu hapa nchini na sio imekaa kimya hapana inashughulikia na tunahakikisha deni hili litalipwa ili wastaafu wetu waweze kuishi maisha marefu bila kupata msongo wa mawazo ambao unaweza ukasababisha kupoteza maisha kabla ya wastaafu hawajapata mafao.” amesema Waziri Profesa Ndalichako.

Ameeleza zaidi kuwa dhamana aliyopewa na raisi ni kubwa ya kutumikia watanzania wakiwemo wastaafu wote hivyo hana budi kufanya kazi kwa juhudi na maarifa kwa kushirikiana na serikali ili kusukuma mbele gurudumu hili la maisha na kutekeleza mpango wa matokeo kwa wastaafu.

Naye mkuu wa Wilaya ya Songea, Kapenjama Ndile amesema kuzinduliwa kwa mpango huo kutasaidia kupunguza kero za wastaafu zinazofanywa na mashirika mbalimbali ikiwemo mifuko mbalimbali ya Hifadhi ya Jamii.

Mmoja wa wastaafu akipokea kitabu cha kumbukumbu za wastaafu

Ndile amewatoa hofu wastaafu ambao walikuwa wamehama mifuko kuwa wasihofu watapata fedha zao zote ambapo mifuko imekuwa ikitoa kiasi cha fedha ambacho mwanachama amekuwa akichangia kwa awamu tofauti basi ni vyema mwanancha apewe kiasi kikubwa cha fedha badalaya kupewa kiasi kidogo cha fedha.

Kwa upande wao baadhi ya wastaafu mkoani humo wameishukuru serikali kwa kuona umuhimu wa kuwalipa pensheni zao kwa wakati tofauti na miaka ya nyuma fedha zao za pensheni walikuwa wanalipwa kwa kuchelewa sana jambo ambalo limeleta matumaini kwa wastaafu wengi.

By Jamhuri