Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia, Dodoma

Mbunge wa Jimbo la Kongwa na Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Job Yustino Ndugai amewaasa Wananchi kufanya kazi kwa bidii na kutuza mazingira kama jitihada za kupambana na Umaskini.

Amesema hali ya umaskini inachangia uharibifu wa mazingira kupitia shughuli za kibinadamu, jambo linalopelekea athari zitokanazo na mabadiliko ya tabianchi.

“Ni tabia ya maskini kuharibu mazingira. Ukimkuta tajiri anakata mti, labda ana faida zake anapata kwa maana labda anatengeneza mbao na atapanda mti mwingine kwa niaba yake” amesema Ndugai.

Ndugai pia ametoa wito kwa Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Mayeka Simon Mayeka kuwasaidia wananchi, kupiga vita umaskini na uharibifu wa mazingira kama kipaumbele kikuu cha kuinua uchumi wa wananchi wa Wilaya ya Kongwa ambao alidai wengi wao wanaishi kwenye hali ya umaskini “Mimi kama mwakilishi wa wananchi nakuomba eneo moja tu la kufanyia kazi; nalo ni maendeleo ya uchumi wa watu wa Kongwa”

Nasaha hizo kutoka kwa Mhe. Ndugai zimetolewa usiku wa Februari, 09, 2024 wakati akitoa salamu zake katika hafla ya kumpa mkono wa kwaheri Mhe. Remidius Mwema Emmanuel Mkuu wa Wilaya aliyehamia Wilaya ya Kiteto, na kumkaribisha Mhe. Mayeka Simon Mayeka, Mkuu mpya wa Wilaya ya Kongwa aliyehamia kutokea Wilaya ya Chunya.

Akizungumza katika sherehe hizo, Mkuu wa Wilaya ya Kiteto Remidius Mwema Emmanuel alisema, ataendelea kuikumbuka Wilaya ya Kongwa kwa mambo mengi ikiwemo ushirikiano wa viongozi uliopelekea ukamilishaji wa miradi ya maendeleo kwa Wakati na kuibuka kuwa kinara ngazi ya Taifa.

Kwa Upande wake Mhe. Mayeka Simon Mayeka Mkuu wa Wilaya ya Kongwa aliwataka wanakongwa kudumisha umoja katika utekelezaji wa shughuli za maendeleo ili kuendeleza kasi ya uwajibikaji katika taasisi mbalimbali.

Sambamba na hilo amewataka wananchi kuunga mkono Jitihada za Serikali katika utunzaji wa mazingira ikiwa ni pamoja na kufanya usafi wa mazingira katika maeneo ya hifadhi za barabara zinazopita katika makazi yao badala ya kuzitegemea taasisi sinazohusika na ujenzi wa barabara.

Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa Mhe. White Zuberi Mwanzalila alisema mchango wa Mhe. Mwema kuhusu kutangaza historia ya harakati za ukombozi wa nchi za kusini mwa Afrika umeanza kuzaa matunda kwani baadhi ya viashiria vimeanza kuonekana ikiwa ni pamoja na kufanyika kwa Ukarabati wa handaki lililotumiwa na wapigania uhuru sanjali na mpango wakufanyika kwa maadhimisho ya siku ya mtoto wa Afrika mwaka 2024, kufanyika Wilayani Kongwa.

Hafla hiyo iliandaliwa na kamati maalumu kwa usimamizi wa Katibu tawala Wilaya Bi. Sozi Ngate ambapo wakuu wote wa wilaya walipewa zawadi mbalimbali kutoka kwa makundi mbalimbali ya kijamii ukiwemo uongozi wa Chama Cha mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kongwa, Wafugaji, Wakulima na watumishi