Mwanafunzi wa shule ya Msingi Chalinze Modern Islamic, Mkoa wa Pwani, Iptisum Slim amedai kubadilishiwa namba yake mtihani wa kumaliza elimu ya msingi Oktoba 5 hadi 6, 2022.

Kupitia video inayosambaa kwenye mitandao ya kijamii mwanafunzi huyo mhitimu wa darasa la saba, amemuomba Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda kuingilia kati madai ya kufanya mtihani na namba ambayo si yake.

Kupitia video hiyo alionekana akiomba msaada huku akieleza, siku ya mtihani wa taifa alivyoingia darasani alipangiwa namba 40 ambayo si yake na wakati karatasi ya kusaini ilivyopita alisaini namba 39 .

“Baada ya mtihani kumalizika baadhi ya wanafunzi tuliitwa na mwalimu mkuu tukaambiwa yale yaliyotokea yasisikike sehemu nyingine yaishie palepale.

“Naomba msaada nisaidiwe kisheria kupata haki majibu yangu yarudi kwenye namba yangu kwa sababu mtoto niliyemfanyia mtihani anashika nafasi ya chini na mimi nashika nafasi za juu hata Mtihani wa Moko wilaya nilishika nafasi ya kwaza,”ameeleza mwanafunzi huyo.

Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA) limesema linafanyia kazi tuhuma alizozitoa mwanafunzi katika taarifa iliyotolewa na Afisa Habari na Uhusiano Necta, John Nchimbi ili mwanafunzi huyo apate haki yake.

“Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) limeona taarifa inayosambaa kwenye mitandao ya kijamii ikimuonesha mtahiniwa Iptisum Suleiman Slim wa Shule ya Msingi Chelinze Modern Islamic ‘Pre and Primary School akisema kwamba alibadilishiwa namba yake ya mtihani wakati akifanya mtihani wa kumaliza Elimu ya Msingi uliofanyika tarehe 5 na 6 Oktoba 2022.

“Baraza linaifanyia kazi taarifa hiyo kuhakikisha mwanafunzi huyo anapata haki yake,”imeeleza taarifa hiyo..

Pia kupitia mtandao wa kijamii wa Instagram, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk Dorothy Gwajima ameandika

“Mtoto wetu mpendwa sana, kwanza pole kwa mtihani, hongera kumaliza darasa la saba. Badala ya kumaliza upumzike wamekutengenezea jambo. Kwa nafasi yako kama mtoto iwapo hili limetokea nao ni ukatili kwa mtoto.

“Waziri wa Elimu na NECTA wapo pamoja na wewe mtoto mzuri kuchunguza hili ili haki itendeke.

“Wizara yenye dhamana na maendeleo ya watoto jicho letu, sikio letu na mguu wetu vipo walipo watoto wanaolalamika kwa chochote hivyo, katika hilo tunaungana na wizara ya Elimu hadi tuone mwisho wa hii hoja” amendika waziri Gwajima.

By Jamhuri