Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia, Dodoma

BARAZA la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limesema lipo mbioni kuanza kufanyia kazi upya mapitio ya Sheria za mazingira ili kufanikiwa, kupunguza na hatimaye kukomesha kabisa uharibifu wa mazingira nchini .

Hatua hii imekuja kufuatia agizo la Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango alilolitoa kwenye kilele cha Siku ya Mazingira Duniani June 5,2024 Jijini Dodoma kuhusu uimarishwaji wa menejimenti na usimamizi wa mazingira ikiwemo kupima na kuzingatia matumizi bora ya ardhi pamoja na kubadili mfumo wa ufugaji ili kulinda mazingira.

Akizungumza na Waandishi wa habari leo June 6,2024 Jijini hapa Afisa Mazingira Mwandamizi wa NEMC Innocent Makomba ameeleza kuwa hali hiyo itasaidia kuleta mabadiliko ikiwa ni pamoja na kuchochea utunzaji wa mazingira wenye tija utakaojenga ustahimilivu dhidi ya ukame na kuzuia kuenea kwa jangwa .

Makomba amesema madhimisho ya Siku ya mazingira Duniani yameleta ari ya kusimamia kikamilifu Sheria zote zinazohusu mazingira ikiwa ni pamoja na kuhakikisha hatua za kisheria zinachukuliwa dhidi ya wanaokwenda kinyume na sheria hizo.

“Baada ya madhimisho haya, kazi imebaki kwetu, tunaenda kuangalia mfumo upya hususani kwa watu wenye viwanda wasiofuata masharti, kuna wale wanao tengeneza vifungashio visivyokidhi vigezo vya ubora, tutawakagua na kuwafikisha kwenye mkono wa Sheria, lengo ni kuona mazingira yetu yanakuwa salama wakati wote,” amesisitiza

Kwa upande wake Pendo Kundya ambaye ni Afisa Mazingira Mkuu wa NEMC ameeleza kuwa watayafanyia kazi maelekezo yote yaliyotolewa na Serikali pamoja na maoni ya wananchi kwa kipindi chote cha maadhimisho ya Siku ya Mazingira kwa kuboresha kwenye mapungufu.

Mbali na hayo ametoa rai kwa wananchi kuendelea kuwa wahifadhi wakuu wa mazingira ili kukabiliana na uharibifu wa mazingira,kuendana na Kauli mbiu ya maadhimisho hayo kwa mwaka huu ambaye ni kuhuisha ardhi iliyoharibiwa, kuzuia kuenea kwa jangwa na kujenga ustahimilivu dhidi ya ukame.

Pamoja na mambo mengine ameeleza kuwa maadhimisho hayo yamehusisha maonesho yenye lengo la kutoa elimu ya utunzaji na uhifadhi wa Mazingira kwa kuambatana na matukio mbalimbali yakiwemo Uzinduzi wa mradi wa urejeshaji uoto wa asili unaotekelezwa wilaya 7 katika Mikoa mitano nchini ambayo ni Iringa, Njombe, Rukwa, Mbeya na Katavi.

Aidha umefanyika uzinduzi wa sera ya Taifa ya uchumi wa buluu ya mwaka 2024 iliyoambatana na ugawaji wa vyeti kwa wadau wa mazingira.