*Asimulia tukio zima la ajali waliyoipata,
aelezea afya yake
*Awashukuru wananchi kwa
kumwombea
*Alitangaza wosia, watu anaowadai na
wanaomdai

Nianze kwa msemo maarufu wa lugha ya
Kiswahili usemao: “Kama haujui kufa,
tazama kaburi.” Anayeweza kuthibitisha
maneno haya ni yule aliyenusurika katika
matukio mabaya ambayo yangeweza
kusababisha kifo.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamis
Kigwangalla, ambaye amenusurika kifo
katika ajali ya gari akiwa katika ziara ya

kikazi mkoani Arusha anasimulia tukio zima
la ajali hiyo na namna alivyonusurika.
Gazeti la JAMHURI linakuletea maelezo
yake neno kwa neno, kama alivyosimulia
kupitia chombo kimoja cha habari. Hapa
chini ni maelezo yake.
Kwanza, napenda kuanza kumshukuru
Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa
kunipa uhai, zawadi kubwa, rehema kubwa
amenipa mpaka hapa.
Pili, naushukuru uongozi wa nchi yetu,
nikianzia kwa Rais wetu, Dk. John Magufuli,
mawaziri wenzangu, wakuu wa mikoa ya
Arusha na Manyara, Katibu Mkuu wa wizara
yangu, Naibu Katibu Mkuu na Naibu Waziri,
Japhet Hasunga.
Kwa nafasi ya kipekee napenda kutambua
mchango wa ndugu yangu, Allan Kijazi,
Mkurugenzi Mkuu wa TANAPA kwa
mchango wake na kusaidia kupatikana kwa
haraka kwa helikopta iliyo ‘respond’ kwa ajili
ya kutusaidia.
Pia shukrani zangu za dhati nazipeleka kwa
ndugu yangu ambaye kwa bahati mbaya

sijamfahamu hata jina mpaka sasa. Ni mtu
ambaye alikuwa wa kwanza kufika eneo la
tukio akiwa na gari dogo aina ya Raum
akitokea Babati kuelekea Arusha akiwa
anawahi shughuli zake.
Alipokuta ajali imetokea, wala hakujua
humo ndani kuna waziri, kwa imani yake
aliamua kuacha gari lake na dereva wake
akasema yeye anawahi shughuli zake huko
na kutuombea kila la heri ili atukimbize
kwenye Kituo cha Afya cha Magugu
ambacho kiko karibu na hapo tulipopata
ajali.
Anasema dereva huyo aliwachukua haraka
sana na kuwakimbiza kwa ‘speed’ ya ajabu
hadi akaogopa kwamba pengine angepata
ajali nyingine.
Ninamshukuru sana dereva huyo
aliyetufikisha Kituo cha Afya cha Magugu,
askari wa Jumuiya ya Uhifadhi wa
Wanyamapori wa Gurunge na baadhi ya
askari wa TANAPA waliofika kwa haraka
sana eneo la tukio na kutusaidia.
Kwa namna ya pekee sana mtu niliyekuwa

naye karibu, kwa sababu tu ni jukumu lake,
ndugu Ramadhan Magumba na dereva
wetu, mzee Juma, kwa namna ya kipekee
ambao waliweza kutoa msaada wa haraka
sana kwangu binafsi kwa kunitoa chini
kabisa ya gari na wakafanikiwa kunitoa nje.
Huyu msaidizi wangu, Magumba, alifanya
jitihada za ziada, kumbe naye alikuwa
ameumia maskini wa Mungu, lakini alifanya
jitihada za ziada kunibeba na kuhakikisha
nimeingia ndani ya gari, pia nimefika
hospitalini na kupata huduma ndipo na yeye
akazimia.
Kwa hiyo alionyesha uzalendo wa hali ya
juu na uimara wa kiaskari kweli kweli,
nimefarijika sana kwa msaada wake. Pia
nimeona umuhimu wa kuwa na wasaidizi
ambao wanaipenda kazi yao na kujitoa kwa
ajili ya kazi yao.
Katika taharuki hiyo, anawashukuru
wahudumu wa Kituo cha Afya cha Magugu
ambao walimpokea yeye na wenzake na
kufanya jitihada za kuokoa maisha.
Dk. Kigwangalla anakumbuka walimwekea

oxygen kwa sababu ya tatizo alilokuwa
amelipata la mapafu na kuvunjika mbavu,
‘the first hour’ na kuweza kuokoa maisha
yake, bila hivyo asingekuwa hai leo.
Ninawashukuru sana kwa umoja wao
wahudumu wa Kituo cha Afya cha Magugu,
waganga na madaktari wakiwemo marafiki
zangu; Damas Juma, Mganga Mkuu wa
Mkoa (RMO) wa Manyara na madaktari
wengine kwa umoja wao na ma- DMO
ambao walinifunga POP ya kwanza.
Watambue kwamba chini ya sakafu ya
moyo wangu nawashukuru sana kwa moyo
wa dhati, lakini pia kwa namna ya kipekee
niwashukuru sana Kilimanjaro SAS
walioleta helikopta yao kwa haraka eneo la
tukio kunichukua mimi na majeruhi
wenzangu na kutupeleka mpaka Arusha.
Zaidi walinipatia hewa ya oxygen na
huduma ya kwanza, angalau nikawa na
matumaini ya kuishi, kabla ya hapo nilikuwa
napigania hewa kwa namna ambayo
nilikuwa na maumivu ya ajabu ambayo mtu
huwezi kuyapata ukiwa hai.

Naweza kusema kwa kweli nimenusa
umauti, karibia kumwona Mungu. Kwa kweli
nimepata fundisho au uamsho wa namna ya
kutafakari maisha, kifo na yale
yanayoambatana.
Napenda kuwashukuru madaktari bingwa
wote wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa
Arusha (Mount Meru) na Seriani, kwa
pamoja walitengeneza timu nzuri sana,
walinihudumia kwa weledi wa hali ya juu
mpaka nikapata moyo kwamba nchi yetu
sasa ina wataalamu na weledi wa kutosha,
nikaamini niko mahali salama.
Dk. Kigwangalla anasema anamalizia katika
hatua hiyo ya awali kwa kuwashukuru sana
madaktari, akiwemo Dk. Hancy, Dk.
Mabula, Dk. Mng’ong’o na wengine ambao
hakuwataja kwa majina kwamba anatambua
msaada waliompa.
Katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili
ninawashukuru sana Dk. Juma Mfinanga,
Dk. Ally Hamis Mwanga ambao walikuwa
mstari wa mbele kuongoza jopo la
madaktari wenzao kunihudumia.

Nawashukuru pia madaktari wote kaka
zangu wa hapa MOI, Dk. Anthony, Dk.
Haonga, Dk. Ndarama, Dk. Mabula, Dk.
Albert na madaktari bingwa wote walioko
hapa akiwemo Profesa Mseru, Dk. Swai,
Dk. Bonny wote kwa pamoja natambua
mchango wenu na pia wote ambao
sijawataja kwa majina.
Natambua sana huduma zote nilizopewa na
wauguzi wote tangu Kitengo cha ICU,
kuanzia kina Lameck Mnyanyu, Martin,
Rashid Majisu na baba mchungaji na
wengine wote ambao bahati mbaya
siwakumbuki kwa majina ambao
wamenigusa na kunihudumia, natambua
mchango wenu mkubwa na kuuthamini.
Hata hivyo anasema kwa bahati mbaya
watu wengi hawakuweza kumwona, lakini
anakiri kupokea salamu zao kwa maandishi,
kadi, ujumbe kwa njia ya matunda na vitu
vingine.
Ninawashukuru sana, sina maneno mazuri
sana ya kusema ila nimetambua na
kuthamini sana mchango wenu katika
kipindi hiki kigumu ambacho nimepitia na

ninaendelea kupitia.
Mimi sina cha kuwalipa zaidi ya kuwaombea
kwa Mungu awabariki sana, Mungu
awaepushe na balaa, awaondolee nuksi,
mikosi, awawekee wepesi kwenye mitihani
mnayokutana nayo.
Mungu wa haki aendelee kuwajaza baraka
mpate neema kubwa kubwa na ndogo
ndogo, muweze kufuzu na kuwa waja wake
wema hapa duniani na kesho pia ahela.
Sina maneno mazuri ya kuzungumza nikiwa
hapa kitandani, lakini kwa kuwa nimeamua
leo kuzungumza kidogo kuhusu jambo hili ni
vema nikaueleza umma ni kwa kiasi gani
nimesikitishwa na msiba wa mdogo wangu,
msaidizi wangu, Hamza Temba, ambaye
alikuwa ni Afisa Habari wa wizara.
Sikufahamiana naye muda mrefu, lakini
tangu nilipoteuliwa kwenye nafasi hii ya
Waziri wa Maliasili na Utalii, nimekuwa
nikifanya naye kazi kwa ukaribu sana,
nimekuwa nikipenda watu wanaofanya kazi,
kwa maana mimi mwenyewe nafanya kazi
kwa bidii.

Mtu yeyote anayekuwa kwenye timu yangu,
lazima awe na uwezo mkubwa wa kufanya
kazi kwa sababu ya kasi yangu.
Nimesikitika sana, Hamza ni miongoni mwa
watu wachache niliofanya nao kazi tangu
nikiwa naibu waziri hadi waziri kamili.
Alikuwa na uwezo mkubwa wa kufanya kazi
kwa ubora sana, kwa habari alizokuwa
anatoa, picha alizopiga na video alizokuwa
anarusha na pia uwezo wa kimwili (physical
fitness), kwa kuwa kazi ninazofanya mimi,
lazima uwe na afya kidogo.
Kwa sababu nakimbia sana au kutembea
umbali mrefu sana. Nazunguka kila kona ya
nchi, kila pori, kila kona ya hifadhi nafika. Ni
mwendo mrefu sana kufika kwenye maeneo
ya hifadhi.
Mimi sipendi kupita kwenye maeneo ya ofisi
au nje nje tu. Napenda kukatisha katikati ya
pori na kutokea upande wa pili ili kuona hali
halisi ya uhifadhi katika mapori yetu.
Mbali na safari ngumu ninazofanya, pia
ninapenda kukagua mipaka ya maeneo
yetu, mpaka kwenye milima tunalazimika

kupanda kukagua mawe ya mipaka.
Mimi Waziri huwezi kuniambia kuwa
‘beacon’ ile kwa mbali, mimi siwezi kwenda
mpiga picha asiende kwa sababu lazima
nipige picha kwenye eneo la tukio.
Hamza alikuwa anaendana na kasi yangu,
alikuwa amemudu kasi hii ninayokwenda
nayo. Ameondoka akiwa ni kijana mdogo
sana.
Sisi Waislamu tunasema; sisi sote ni wa
Mungu na kwa Mungu tutarejea, tuko
nyuma yake, safari hiyo ni ya kwetu sote
hata kama tutapenda namna gani tuendelee
kuwa naye, Mungu aliandika safari yake
itaishia hapo na imeishia hapo.
Tunasikitika na kuhuzunishwa sana lakini
tunamwombea dua kwa Mwenyezi Mungu
ampe kauli thabiti huko alikoenda, pia
Mungu amtie nguvu mke wake, mtoto wake
na familia nzima ambao wamebaki hapa
duniani na sisi tunawaahidi familia ya
Hamza kwamba tutaendelea kuwa karibu
nao katika utekelezaji wetu na katika
maisha yetu ya kila siku ili wasijione wakiwa

sana kwa sababu tuliishi vizuri sana na
Hamza alikuwa sehemu ya familia, si tu
kama mfanyakazi mwenzetu.
Sisi sote kama wafanyakazi bila kujali cheo
cha mtu, tunaishi kama familia,
tunapendana, tunaelewana na kushirikiana.
Kwa hiyo mwenzetu mmoja ametangulia,
familia yake tunaiona kama familia yetu sisi
tuliobaki.

Kuhusu afya

Anasema anaendelea vizuri na matibabu na
yuko katika hatua nzuri kwa sababu mapafu
yamerudi katika uwezo wake wa kufanya
kazi kama kawaida na vipimo vyote
vinaonyesha kuna tatizo dogo kwenye
mapafu.
Dk. Kigwangalla anasema kidonda
ambacho kipo kwenye eneo walilopitishia
mpira wa kutolea uchafu ndani kimetolewa
nyuzi na sasa kimeanza kupona, kitapona
katika muda mfupi ujao.

Tatizo kubwa ambalo nimebaki nalo ni
mkono, ambao nao umeshafanyiwa
upasuaji, kwa siku kama tano hivi nitaanza
kuufanyia mazoezi. Nikianza mazoezi
nitakuwa nimefika katika hatua nzuri,
pengine kuanza kufanya kazi kidogo kidogo,
lakini nimekusudia kuwaomba madaktari
wanipumzishe.
Pamoja na hayo, anasema kitakuwa ni
kipindi cha kutafakari mustakabali wa
maisha yake na utekelezaji wa majukumu
yake kama waziri ndani ya serikali.
Kabla ya kupata ajali alikuwa tayari
amefanya ziara ya zaidi ya mwezi mmoja na
nusu na kujionea changamoto mbalimbali
na kutoa maagizo na ushauri kuhusu
mambo mbalimbali ambayo baada ya afya
yake kuimarika atakuwa na wasaa wa
kuyafanyia kazi.
Utakuwa ni wakati wa kuanza utekelezaji
wa bajeti kwa mwaka wa fedha unaofuata,
hayo ndiyo yatakuwa majukumu yangu.
Baada ya ajali hii tumeamini kuwa kuna
Mungu hata kama tulikuwa tunaamini kwa
wastani, sasa baada ya ajali hii tunaamini

kwamba Mungu yupo.
Tumeiona nguvu ya Mungu, pia tumeiona
huruma ya Mungu. Tumeona jinsi mtu
anavyoweza kuamka na mipango yake
mingi, lakini kwa ghafla anakutana na ajali
na wengine kupoteza maisha.
Mwanadamu hajui ni lini ataondoka na
sababu ya kifo chake. Mfano mimi
mwenyewe kabla ya dakika tatu kupata ajali
nilikuwa namuuliza swali katibu wangu,
lakini hakunijibu na dereva akasema hao
wote wamelala.
Tuliokuwa macho ni mimi, dereva na mpiga
picha za video, wakati huo nilikuwa nachati
kwenye group letu na rafiki zangu madaktari
ambao tumesoma pamoja.
Niligeuka nyuma kumuuliza katibu wangu
na baada ya kurudisha macho yangu mbele
niliona kuna twiga, dereva alifunga breki kali
na kuachia ili kumkwepa yule twiga.
Muda mfupi baada ya kumkwepa, nikaona
gari limepaa kama vile ndege ina ‘take off’
nikasema hii si hali ya kawaida ni ajali na
dereva alikuwa anaomba dua, nami pia

nikaomba dua zangu na kutoa shahada
huku nikijua kuwa tunakwenda kufa tu.
Wakati huo naangalia gari lilivyokuwa
likipaa na chini kuna bonde, sikuelewa
chochote kilichotokea baada ya hapo hadi
gari lilipotulia ndipo nikasikia sauti za
wasaidizi wangu wakiniita na kuniuliza
kama niko salama.
Nilipoitika kwamba niko salama, nafumbua
macho hivi siwezi kuona kitu chochote, ila
nasikia sauti zao huko nje wakiitana majina.
Akili zangu zote ziko timamu, najitahidi
kufumbua macho lakini sioni kitu, nikasema
labda pengine nimekwisha kufa. Nikawa
nasubiri kitakachoendelea.
Nikaona mtu amenishika mkono na bega
akinivuta huku nikiwa nasikia maumivu hadi
nikasikia nimetoka nje. Damu zilikuwa
zinatoka puani na mdomoni, siwezi kukaa,
kusimama, mkono hauwezi kushika, siwezi
kupumua na kutoa sauti hapo nikajua muda
wowote naondoka.
Kutokana na hali hiyo nikamwita msaidizi
wangu ili nimpe wosia wa kufikisha kwa

mke wangu na watoto wangu, mimi safari
imetimia.
Lakini Mungu alikuwa na mipango yake,
bahati nzuri sikuweza kuondoka,
nikavumilia kwa muda wote huo nikipumua
kwa shida hadi niliposafirishwa kwenye
Kituo cha Afya cha Magugu na kutoka hapo
hadi Arusha na hatimaye Dar es Salaam.
Muda wote huo nilikuwa naomba dua zangu
za mwisho. Hata nilipompigia simu mke
wangu nilimwambia haya huenda ni
maneno ya mwisho kati yangu na wewe.
Nikampa pia maagizo kwa watoto wangu,
pia msaidizi wangu nilimtajia watu ambao
nawadai na wale wanaonidai kwamba
ahakikishe hilo analisimamia kama yeye
atakuwa amevuka.
Mpaka jioni nafika hapa Muhimbili nilikuwa
naona kwamba siwezi kuendelea kuishi, leo
hii naweza hata kuzungumza. Huu ni
muujiza tu, kwa hiyo namshukuru sana
Mungu kwa rehema hizi alizonipa.
Nimejifunza kama nilivyoandika siku yangu
ya kuzaliwa kwenye ukurasa wangu wa

Instagram kwamba pengine Mungu
ameniacha niwe hai ili niweze kuutangaza
utukufu wake.
Pengine ni fursa ambayo nimepata niseme
Mungu Mkubwa, anasamehe na sisi
wanadamu tumwabudu Mungu, tuishi kwa
kufuata maadili na kutenda wema kwa
sababu hatujui siku wala saa ambayo
Mungu atatuita.
Kila wakati mwanadamu unapaswa
ujiandae, uwe tayari kwa sababu kifo
kinakuja wakati wowote na kwa namna
yoyote ile.
Kama ajali tuliyopata sisi huwezi kusema ni
kosa la dereva au mtu yeyote, ni ajali
ambayo haumlaumu mtu yeyote. Katika
mazingira ya namna hiyo ambayo Mungu
anakupa nafasi nyingine ya kuishi (second
chance) inabidi kujitafakari sana.
Lazima kujitafakari na kujua makusudi hayo
ya Mungu ni yepi na kuyatendea kazi kabla
ya kuitwa na Mwenyezi Mungu kwa kuwa
haujui siku ulizoongezewa kuishi ni ngapi.
Sasa hivi niko katika hatua ya mazoezi

taratibu, nawashukuru pia wale
waliojitokeza kutuona tangu pale tulipokuwa
katika Kituo cha Afya cha Magugu, Arusha
ambako umati mkubwa wa watu walikuja
baada ya kuguswa na ajali iliyotupata.
Pia pale uwanja wa ndege walifika watu
wengi kutupokea na hapa Muhimbili
walijitokeza watu wengi na bahati mbaya
sana wengi walijitokeza tena siku ya pili
lakini hawakuruhusiwa kuniona nikiwa ICU.
Wote hawa kwa upendo wao mkubwa na
nia yao ya dhati kutujulia hali nawashukuru
sana. Naomba pia wazisamehe mamlaka
za madaktari na serikali waliozuia kuniona,
ndiyo maana nimeamua kutoa taarifa hii ili
watu wapate moyo kwamba naendelea
vizuri.
Watu walikuwa wamezuiwa kuniona kwa
sababu za kitabibu na kiusalama, hivyo
nimependa nilizungumzie na hili ili wajue
kuwa salamu zote nilikuwa nazipata kwa
kila aliyefika.
Kila mmoja aliyefika nilikuwa napata taarifa
zake kwa kuambiwa fulani alifika kukuona

na jina lake liliandikwa. Nashukuru sana
kwa kuja kuniona, nafahamu ni ndugu
zangu, rafiki zangu, watumishi wenzangu,
viongozi wenzangu wasijisikie vibaya
kwamba hawakuweza kuniona.
Hali yangu ililazimisha madaktari waamue
hivyo na hata kama wangeruhusiwa
wasingeweza kuzungumza nami kwa
sababu nilikuwa nachomwa dawa kali za
usingizi na maumivu na muda mwingi
nilikuwa nalala.
Uamuzi huo ulikuwa ni jambo la busara kwa
madaktari na mamlaka za serikali kuzuia
watu kuniona kila wakati, hata mawaziri
wote wamezuiliwa kuniona, wengi walikuja
kuniona, natambua upendo na mshikamano
waliokuwa wameuonyesha.
Pia natambua kuwa wajumbe wenzangu wa
Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) walikuja
kwa wingi kuniona, lakini nao walizuiwa.
Natambua mshikamano wao na watu wote
waliofika kunijulia hali, Mungu awabariki
sana.

Mwisho

Please follow and like us:
Pin Share