Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia

Shirika la Bima la Taifa (NIC) limeelezea mageuzi yaliyofanyika ndani ya miaka mitatu katika shirika hilo na kusababisha litoke kwenye kuzalisha hasara na kuzalisha faida.

Katika kipindi cha mwaka 2019/20 NIC ilikua inazalisha faida ya Sh bilioni 33.6 lakini mwaka 2020/21 faida iliongezeka na kufikia Sh bilioni 63.21 sawa na ongezeko la asilimia 43.6 Kwa mwaka.

Hayo yameelezwa na Mkurugenzi Mtendaji wa NIC, Dk Elirehema Doriye wakati akizungumza na wahariri na waandishi wa Habari kwenye kikao kilichoandaliwa na Ofisi ya Msajili.

Amesema kwa muda wa miaka 30 shirika hilo lilikuwa halijawahi kutoa gawio serikalini lakini ndani ya miaka mitatu limetoa kiasi kinachofikia Sh bilioni 13.

“Kabla ya mwaka 2019 ukweli ni kwamba shirika lilikuwa na hali mbaya ya madeni, linazalisha hasira na likijiendesha bila kuzingatia teknolojia. Lilikuwa katika hatihati ya kufutwa na msajili,” amesema.

Amesema kutokana na mageuzi hayo ndani ya shirika hadi kufikia Juni, 2022 NIC ililipa madeni ya wateja kumpa Sh bilioni 33.7 wa bima ya Maisha na Sh bilioni 40.1 wa bima za ajili na mali.

“Kutokana na hali mbaya tuliyokuwa nayo tulikuwa na malimbikizo ya madeni. Tukaamua tuanze kuwatafuta wanaotudai kuazia mwaka 1994. Nasimama hapa leo kuwahakikishia hatudaiwi na mtu yeyote kuanzia 1994,” alisisitiza Dk Doriye.

Amesema mali za shirika hilo zimeongezeka na kufikia Sh bilioni 423.9 na sehemu kubwa ya mali hizo inaweza kugeuzwa fedha wakati wowote.

Aidha, amesema mtaji wa NIC wa wanahisa ambao ni serikali umeongezeka kutoka Sh bilioni 72 mwaka 2019/20 hadi Sh bilioni 217 mwaka 2021/22 sawa na ongezeko la asilimia 100.

Dk Doriye pia amesema kwa sasa asilimia 13 ya mapato ya shirika hilo yanatokana na mfumo wa kidijitali.

Amesema katika eneo la mapato baada ya kuondokana na shirika hilo kutengeneza hasara mapato yameongezeka kutoka Sh 76.45 mwaka 2019/20 hadi Sh bilioni 103.94 mwaka 2021/22.

Pamoja na hayo, mkurugenzi huyo alisema katika kipindi hicho cha miaka mitatu huduma za NIC Kwa wateja zimeboreshwa na malipo kwa mteja yanafanyika ndani ya siku saba kutoka siku 35 hadi 45.

Amesema kutokana na mafanikio hayo yote ukuaji wa shirika hilo ni wa asilimia 108 huku likimiliki soko la bima Kwa asilimia 16.

Alitaka hata za mageuzi zilizosababisha mafanikio hayo ya NIC kuwa ni kubadilisha uongozi, kuzingatia ufanisi na weledi, kuzingatia tija, rasilimali watu na uwekezaji kwenye mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).

Dk Doriye amesema NIC katika kujiboresha zaidi limejipanga kutoa elimu ya bima Kwa Watanzania Kwa kwa utafiti uliofanyika mwaka 2018 unaonesha ni Watanzania asilimia 36 tu ndio wana uelewa wa bima za kati yao asilimia 15 ndio wanatumia bima.

KUHUSU NIC

NIC Insurance ni kampuni inayomilikiwa na Serikali kwa 100%, ikiwa na dhamana ya kufanya biashara ya bima za mali na ajali pamoja na bima za Maisha.

kati ya makampuni zaidi ya 30 yaliyopo kwenye soko la bima Tanzania, NIC insurance imeweza kumudu ushindani huu kwa kufanya vizuri baada ya maboresho mbalimbali yaliyofanyika tangu mwaka 2019.

MABADILIKO YA UTENDAJI

NIC Insurance imekuwa ikitekeleza shughuli zake kwa kuzingatia mwongozo wa uanzishwaji wake (“MEMART”) na Sheria ya Bima Na. 10 ya mwaka 2009.

NIC insurance ilianza kuchukua hatua za mabadiliko ya kiutendaji ili kujiimarisha kibiashara na tangu Julai 2019.

By Jamhuri