Nitaifanyia‌ ‌nini‌ ‌nchi‌ ‌yangu?‌

Kila kukicha, kila eneo ninakopita nasikia watu wakilalamika na‌kusema nchi yao haijafanya hiki, au serikali haijawafanyia kile. Lakini je, ni watu wangapi wanawaza kufanya kitu fulani kwa ajili ya nchi yao?‌

Ni mara ngapi umewaza kuifanyia kitu kikubwa Tanzania? Ni mara ngapi umewaza‌ kuifanyia kitu kikubwa nchi yako? Tusiwe‌watu wa kukaa na kuwaza nchi yetu itatufanyia nini, bali sisi tutaifanyia‌ nini nchi yetu. Ndoto yako ibebe kitu ambacho kwa namna moja au nyingine kitakuwa na mchango kwa nchi yako.

Aliyewahi kuwa Rais wa Marekani, John F. Kennedy siku moja akitoa hotuba kwa wananchi alisema,‌ “Wamarekani wenzangu, msiulize nchi yenu itawafanyia nini, bali‌ mjiulize mtaifanyia nini nchi yenu.”

Siku si nyingi zilizopita nilisikia binti mmoja akitoa mchango wake katika jukwaa la fikra ambalo lilikuwa likijadili namna ya kuikuza elimu ya Tanzania. Binti huyo alisema, “Tunaomba serikali itusaidie‌ mawazo yatakayotusaidia kujiajiri.”

Sikukubaliana na binti huyo kwa sababu moja kuu – alitanguliza kufanyiwa kazi na serikali wakati yeye hajaifanyia kitu serikali. Hata hivyo, serikali haiwezi kukupa mawazo ya kutoka kimaisha kama wewe bado kichwa chako hakijajenga mawazo hayo.

Orville na Wilbur Wright walikuwa na ndoto ya kupaa angani.Walijua mioyoni mwao kwamba jambo hilo linawezekana. Hawakuwa na pesa, hawakuwa na‌ msaada wowote kutoka kwingine, na kibaya zaidi hawakuwa na elimu ya chuo. Katikati yao kulikuwa na kiu ya wao kutimiza ndoto yao. Hatimaye Desemba‌ 17,  1903‌ wakawa watu wa kwanza kupaisha ndege angani ingawa iliruka futi 12 kwa muda‌ wa sekunde 12 tu.

Kitu cha kujifunza katika stori hii ni kwamba kuna mtu‌mwingine ambaye aliitwa Samuel Pierpont‌ Langley, huyu ndiye watu walijua atakuwa mtu wa kwanza kuipaisha ndege. Walidhani ndiye atakuwa‌ mvumbuzi wa ndege. Serikali ya Marekani ilimpa dola 50,000 za‌ nchi hiyo ili atimize jambo hilo,‌hivyo kwake pesa haikuwa tatizo katika matatizo yake.

Magazeti makubwa kama The New York Times muda wote yalitembea naye kila kona wakiandika makala nyingi zilizomhusu; na dunia nzima ilikuwa ikisubiri kwa shauku kubwa Langley azindue ndege ya kwanza. Baada ya ndugu wawili kupaa angani, Langley akafunga makabrasha yake pamoja na vifaa vyake vyote. ‘Biashara‌’ ikaishia hapo. Hakuwa na kiu ya kufanya mambo makubwa, alitaka kujulikana na kuwa tajiri kupitia kupaisha ndege. Hakuwa mtu wa kusema ataifanyia nini nchi yake, bali nchi imfanyie nini. Ndiyo maana hujawahi kusikia chochote kingine kinachomhusu.

Kumbe Serikali inaweza kukupa kila kitu, lakini kama huna nia ya kufanya kitu huwezi kufika popote.

Usiwe mtu wa kusubiri nchi ikupe mawazo ili utoke kimaisha. Kuwa mtu wa kuipa nchi mawazo ili itoke‌ ilipo leo na kufika mahali pakubwa.

Yusufu alichaguliwa kuwa Waziri Mkuu wa Misri kwa sababu moja kubwa; alionekana kuwa mtu mwenye uwezo wa kuipitisha nchi katika misukosuko ambayo ilikuwa inakaribia kuikumba.

Yusufu alijua nchi itapita katika miaka 7 ya mavuno na miaka 7 ya njaa, hivyo alitoa ushauri wakati wa miaka 7 ya mavuno chakula kitunzwe katika maghala ili kisaidie kuikomboa nchi wakati wa miaka 7 ya njaa. Kwa sababu Yusufu aliitafsiri ndoto hiyo vyema, Farao akamchagua  awe kiongozi kwani aliweza kutafsiri ndoto iliyowashinda watu wengi.

Kuna wakati ukafika, dunia nzima ikapatwa na baa la njaa. Chakula kilipatikana Misri‌ pekee. Kila nchi ikaitegemea Misri ili ipate chakula cha kuwalisha wananchi wake. Hata nduguze Yusufu ikawapasa waende Misri kununua‌ chakula. Yusufu akaiokoa familia yake isife kwa njaa.

Najaribu kufikiria Yusufu alikuwa na akili gani ya ajabu ya kutengeneza maghala yanayoweza kutunza chakula kwa miaka 7‌kisiaribike! Huyu alikuwa mtu aliyetanguliza nchi yake mbele na si kujitanguliza yeye.

Ndoto yako isiishie katika kutanguliza nchi yako tu, bali hata jamii inayokuzunguka. Utaifanyia nini‌ familia yako? Utaifanyia nini ofisi yako? Utaufanyia nini mtaa wako?

Siku zote tanguliza nchi yako kwanza, jamii yako kwanza, na wewe ndipo ufuate. Ukifanya hivyo utafika mahali pakubwa sana.

By Jamhuri