Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia

Katika jitahada za kuunga mkono jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita kutatua changamoto kwenye Sekta ya Elimu, Benki ya NMB, imekabidhi misaada ya viti na meza zake 134, madawati 200 na mabati 400 kwa shule tisa (Msingi na Sekondari) wilayani Ilala jijini Dar es Salaam, vyote vikiwa na thamani ya Sh. Mil. 51.3.

Msaada huo ni sehemu ya utaratibu wa NMB kupitia Programu ya Uwajibikaji kwa Jamii (CSR), ambako kwa miaka nane Sasa imekuwa ikitoa asilimia moja ya faida yake kwa jamii, kusaidia utatuzi wa changamoto katika nyanja za elimu, afya na majanga, ambako mwaka huu imetenga zaidi ya Sh. Bil. 6.2.

Makabidhiano hayo yamefanyika leo Alhamisi Agosti 17, 2023 kwenye viwanja vya Shule ya Msingi Mtakuja, iliyopo Vingunguti jijini Dar es Salaam, ambako Meneja wa NMB Kanda ya Dar es Salaam, Dismas Prosper, alimkabidhi Mkuu wa Mkoa (RC), Albert Chalamila, ambaye aliikabidhi kwa Mkuu wa Wilaya ya Ilala (DC), Edward Mpogoro, aliyekabidhi pia kwa walimu na wakuu wa shule husika.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo,Prosper alisema madawati 200 yenye thamani ya Sh. Mil. 20, yametolewa na benki yake kwa Shule za Msingi Mtakuja, Miembeni, Vingunguti na Kombo zilizo katika Kata ya Vingunguti, huku mabati 400 yenye thamani ya Sh. Mil. 13.3 yakienda kwa Shule ya Msingi Airwing na Shule ya Sekondari Kerezange.

“Aidha, viti na meza zake 100 vyenye thamani ya Sh. Mil. 10 tunazitoa kwa ajili ya wanafunzi wa Shule za Sekondari Kivule na Gerezani, huku viti na meza zake 34 vyenye thamani ya Sh. Mil. 8.3 vikiwa ni maalum kwa ajili ya walimu wa Shule ya Msingi Bonyokwa.

“Hii inafanya thamani ya jumla ya msaada huu tunaokabidhi leo kuwa Sh. Mil. 51.3, kiasi ambacho ni sehemu ya Sh. Bilioni 6.2, tulizotenga kurejesha kwa jamii mwaka huu wa 2023 katika Sekta za Elimu, Afya, Majanga na Mazingira, ambako kwa miaka nane sasa tumekuwa na utaratibu wa kurejesha kwa jamii amii asilimia moja ya faida yetu.

“Tunasukumwa na ukweli kwamba jamii ndio msingi mkuu wa mafanikio yetu kama taasisi, wao ndio waliotufikisha hapa, tunapoongoza Sekta ya Fedha nchini.

“Lakini pia dhamira yetu ni kuunga mkono juhudi za Serikali ya Rais Samia katika kutatua kero mbalimbali kwenye nyanja hizo,” alibainisha Prosper huku akiwashukuru walimu wa shule hizo kwa kutambua kuwa NMB ni sehemu sahihi ya kupeleka changamoto zao,” amesema.

Kwa upande wake, RC Chalamila aliishukuru NMB kwa namna inavyotumia vema fungu la CSR katika kuiunga mkono Serikali, ambayo inahitaji sana sapoti ya wadau kufanikisha sera ya Elimu Bure kwa Shule za Msingi na Sekondari inayotolewa na Rais Samia kote nchini.

“Kwa hakika tunawapongeza sana NMB na kuwashukuru kwa misaada yenu hii, fikisheni Salam za Serikali kwa Afisa Mtendaji Mkuu (Ruth Zaipuna), pongezi pia kwa Meneja wa NMB Kanda ya Dar es Salaam, kwa kazi nzuri inayofanywa na benki yenu kwa jamii,” alisema RC Chalamila huku akiwataka wanafunzi wa Shule ya Msingi Mtakuja na nyingine kuitumia vema misaada hiyo kwa kujisomea na kuongeza ufaulu.

Kabla ya makabidhiano hayo, wanafunzi wa Shule ya Msingi Mtakuja walifanya igizo lililoakisi changamoto zao, ambako walisema shule hiyo yenye zaidi ya wanafunzi 2,100 chini ya Mwalimu Mkuu, Magreth Kaiza, ina uhaba wa vyoo, madawati, uzio, na uchakavu wa vyumba vya madarasa, hivyo kuishukuru NMB kwa msaada wao, huku wakiomba wadau zaidi kujotokeza kuwasaidia.


Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam , Albert Chalamila akipokea vifaa mbalimbali kutoka kwa Meneja wa Benki ya NMB Kanda ya Dar es Salaam  Dismas, Prosper vilivyotolewa  kwa Shule za msingi 9 za jijini Dar es Salaam vikiwemo, madawati, viti na Meza pamoja na Mabati
8 na 10
Mkuu waa Mkoa wa Dar es Salaam , Albert Chalamila (katikati) akipiga makofi baada ya kupokea vifaa mbalimbali kutoka kwa Meneja wa Benki ya NMB Kanda ya Dar es Salaam , Dismas, Prosper vilivyotolewa  kwa Shule za msingi 9 za jijini Dar es Salaam vikiwemo, madawati, viti na Meza pamoja na Mabati. aliyekaa ni Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mtakuja, Magreth Kaiza

By Jamhuri