Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Morogoro

WANANCHI wa Mji wa Dumila wilaya ya Kilosa wameondokana na adha ya kutembea umbali mrefu kati ya kilometa 35 hadi 70 kufuata huduma za kibenki, baada ya benki ya NMB kufungua tawi la NMB Dumila.

Akizungumza katika uzinduzi wa tawi hilo, Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara wa Benki ya NMB, Filbert Mponzi amesema wananchi wa Dumila na vijiji vinavyoizunguka walikuwa wakilazimika kusafiri umbali wa kilometa 35 kwenda Mvomero kufuata huduma za kibenki wakati kwenda Gairo kilometa 50, Kilosa kilometa 69 na Turiani kilometa 70.

Aliongeza kuwa, kufunguliwa kwa tawi hili inafanya NMB kuwa na matawi 231 nchi mzima na kuendelea kuongoza kwa kuwa na matawi mengi kuliko benki yoyote hapa nchini na kuishi maana halisi ya kauli mbiu yao ya NMB Karibu yako.

Mgeni rasmi katika ufunguzi huo Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima alisema, benki hiyo inawafikia wananchi wengi na kuwaomba wananchi kutumia benki hiyo, kwa sababu Dumila ina shughuli nyingi za kiuchumi ikiwemo kilimo na ufugaji.

Malima alisema, uwepo wa tawi hilo katika Mji wa Dumila utaongeza tija kwa wakulima kupata mikopo ya kilimo lakini na wafugaji kupata mikopo ya kunenepesha mifugo, ili jamii inayoizunguma benki hiyo kunufaika kihuduma na kubadilika kiuchumi kwa mitaji yao kukua kwa sababu, Dumila sasa ni Mji wenye shughuli nyingi za kiuchumi kwa kukuza biashara zao.

Malima alisisitiza kuwa Dumila ni miongoni mwa miji ya kibiashara unaokua kwa kasi na kwamba ukubwa wa mtandao wa NMB, uimara wake kimapato na huduma rafiki kwa wateja, vinaenda kuneemesha na kuwastawisha kiuchumi wafanyabiashara, wajasiriamali, wakulima na wafugaji wa kada zote watakaotumia fursa hiyo.

Alimaliza kwa kuipongeza NMB kwa lengo lake la kukopesha kiasi cha Sh. Bilioni 1 kwa wajasiriamali, wafanyabiashara, wakulima na wafugaji kwa mwaka wa kwanza, huku akiwataka wana Dumila, Kilosa na Morogoro kwa ujumla, kuchangamkia fursa za ujio wa tawi hilo alilolitabiria kuwa kinara kimafanikio kuliko matawi yote ya mkoa huo.

Wakati huohuo, Benki ya NMB kupitia sera yake ya uwajibikazi kwa jamii, imetumia fursa hiyo kutoa meza 30 na viti 30 kwa ajili ya walimu wa Shule ya Sekondari ya Sokoine na madawati 53 kwa shule ya Msingi Kwadoli vyote vikiwa na thamani ya Sh. Milioni 11.

Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mhe, Adam Malima (wa tatu kulia), akikata utepe kuashiria uzinduzi rasmi wa Tawi jipya la Benki ya NMB Dumila lililopo mkoani Morogoro, wengine katika picha ni Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Shaka Hamdu Shaka (wa tatu kushoto), Afisa Mkuu Wateja Binafsi na Biashara wa Benki ya NMB, Filbert Mponzi (wa pili kulia), Mkuu wa Idara ya Masoko na Mawasiliano wa Benki ya NMB, Rahma Mwapachu (kulia), Meneja Uendeshaji Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Dodoma, Lilian Silaa (kushoto) na wa pili kushoto ni Meneja wa NMB Kanda ya Kati, Janeth Shango.

Sehemu ya wageni waalikwa Waliohudhuria uzinduzi wa Tawi la NMB Dumila.

Meneja Tawi la NMB Dumila, Innocent Kato alimwelezea Mhe, Adam Malima kuhusu huduma zilolewazo na Tawi la NMB Dumila baada ya uzinduzi rasmi

By Jamhuri