Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Arusha

Serikali imezitaka taasisi zilizopewa mamlaka ya upimaji kuhakikisha zinashirikiana na Wizara ya Ardhi pale zinapokwenda uwandani ili kusaidia kuondoa migogoro inayoweza kuanzishwa kutokana na kutojua uhalisia wa mipaka.

Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Geofrey Pinda tarehe Novemba 23, 2023 jijini Arusha wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Mwaka pamoja na Kongamano la Taasisi ya Upimaji Tanzania (IST).

“Hapa mna wataalamu, wapima kutoka TAZARA, Mamlaka ya Reli na maeneo mbalimbali, mtumza ardhi mkuu ni Wizara ya Ardhi kwa hiyo tunatoa wito kwa taasisi hizo zinapokwenda uwandani zifanye mawasiliano na wizara ili kumbukumbu zinazokwenda kufanyika pale ziweze kuwa na uwiano.

Aidha, Mhe Pinda alitoa shukurani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzani Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa upendekeo kwa wizara ya ardhi hususan katika kuridhia miradi mikubwa ya maboresho ndani ya wizara.

Vile vile, aliwaambia washiriki wa mkutano huo kuwa wizara ya Ardhi imeanza kujenga mfumo wake wa TEHAMA wenye lengo la kufanya maboresho yatakayowezesha kuwa na ardhi kiganjani ili kuondoa changamoto za sasa kama vile uwepo viwanja pandikizi sambamba na kuwezesha wananchi kupokea taarifa pamoja na kuwasilisha malalamiko na maombi ya viwanja kupitia ardhi mtandao jambo alilolieleza litaondoa vishoka

“Nitoe wito na angalizo kwa taasisi na makampuni binafsi tuendako tunaenda katika ardhi mtandao muwe karibu na wizara ili kuwa sambamba na mabadiliko haya” alisema Pinda.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Upimaji na Ramani wa Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mansoor Hamdoun amesema, wizara ya Ardhi inaendeea na mikakati ya kuhakikisha inaboresha huduma zinazotolewa na wizara ikiwemo sehemu ya idara ya upimaji na ramani aliyoieleza kuwa ni idara kongwe katika wizara hiyo.

Ametanabahisha kuwa, ipo miradi mikubwa miwili ukiwepo wa ule wa milki salama za ardhi unaotokana na mkopo wa Benki ya Dunia aliouleza kuwa unatarajia kuleta mageuzi makubwa katika sekta ya ardhi ikiwemo eneo la upimaji na ramani.

Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Taasi ya Wapima Tanzania (IST) unashirikisha wataalamu wa upimaji na ramani kutoka wizara ya ardhi, taasisi za umma pamoja na kampuni binafsi ambapo mbali na mambo mengine mkutano huo utatumika kufanya uchaguzi wa viongozi wa Taasisi hiyo.