Na Mwamvua Mwinyi,JamhuriMedia,Pwani

Watu watatu Mkoani Pwani wakiwemo Polisi wawili wamefariki dunia pamoja na mmoja kujeruhiwa ,baada ya gari lenye namba za usajili T.323 BAL aina ya Toyota Crester likiendeshwa na mkaguzi waPpolisi Ndwanga Dastan kuacha njia kisha kugonga karavati,na kusababisha vifo hivyo.

Kamanda wa Polisi mkoani Pwani Pius Lutumo, ameeleza, ajali hiyo imetokea Machi 5, mwaka huu ,majira ya 11:45 alfajiri huko maeneo ya Mavi ya Ng’ombe, Kijiji cha Mboga, Kata ya Msoga, Tarafa ya Chalinze, Wilaya ya Kipolisi Chalinze, barabara ya Chalinze/Segera Mkoa wa Pwani.

Askari Polisi aliyefariki katika ajali iliyotokea Maeneo ya Mavi ya Ng’ombe

“Katika ajali hiyo mkaguzi msaidizi wa Polisi Ndwanga Dastani (28), askari wa kituo cha Polisi Chalinze, akitokea Chalinze kuelekea Lugoba, aliyokuwa akiiendesha liliacha njia kutoka upande wa kushoto wa barabara na kwenda upande wa kulia na kugonga karavati kisha gari hilo kupinduka na kusababisha vifo vya watu wa tatu pamoja na majeruhi mmoja na uharibifu wa gari hilo”

Amewataja waliofariki kwenye ajali hiyo ni Mkaguzi Msaidizi wa Polisi Ndwanga Dastani miaka 28 – aliyekuwa dereva wa gari,Polisi Konstebo Emmiliana Charlse miaka 26 – askari wa kituo cha Polisi Chalinze, na Karimu Simba miaka 27 – karani wa mahakama ya Wilaya ya Lugoba.

Lutumo ameeleza,majeruhi wa ajali hiyo ni Polisi Konstebo Mwanaidi Shabani miaka 25, askari wa Kituo cha Polisi Chalinze ambaye ameumia maeneo mbalimbali ya mwili wake na amepelekwa katika Hospital ya Taifa ya Muhimbili kwa matibabu zaidi.

Amesema,uchunguzi wa awali umeweza kubaini,chanzo cha ajali hiyo ni mwendokasi na dereva kushindwa kulimudu gari na kupinduka.

Lutumo ameeleza ,miili ya marehemu imehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhi maiti katika Hospitali ya Lugoba.

Picha za Polisi wawili marehemu waliofariki katika ajali iliyotokea Maeneo ya Mavi ya Ng’ombe, pamoja na gari ambayo imeharibika vibaya baada ya ajali hiyo.

Askari Polisi aliyefariki katika ajali iliyotokea Maeneo ya Mavi ya Ng’ombe

By Jamhuri