Tanzania miongoni mwa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa zilizosaini na kuridhia mikataba, Itifaki, Maazimio na Makubaliano mbalimbali ya kuzuia uzagaaji wa silaha ndogo na nyepesi.

Moja ya makubaliano hayo ni yaliyofanyika mwezi Julai 2018 kuhusu udhibiti wa uzagaaji wa silaha haramu.

Uzagaaji wa silaha haramu duniani umekuwa ukisababisha uvunjifu wa amani , ukosefu wa usalama na kusababisha hofu kwa watu, vifo na majeruhi. Kutokana na madhara hayo, nchi wanachama walikubalina mwezi Septemba uwe ni mwezi wa usalimishaji wa silaha haramu.

Katika kutekeleza makubaliano hayo, Tanzania kupitia Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhandisi Hamad Yusuph Msauni (MB) kupitia Tangazo la Serikali Na. 619 la tarehe 15 Agosti, 2023 ametoa msamaha wa kutokushitakiwa kwa mtu yeyote atakaye salimisha silaha ambayo anaimiliki kinyume cha sheria.

Msamaha huo umetolewa kufuatia Mamlaka aliyopewa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi chini ya Kifungu cha 64 cha Sheria ya Udhibiti wa Silaha na Risasi ya Mwaka 2015, Sura ya 223. Masharti ya usalimishaji wa silaha haramu kwa hiari ni kama ifuatavyo:

Usalimishaji wa silaha haramu kwa hiari nchi nzima utaanza tarehe 01 Septemba, 2023 hadi 31 Oktoba, 2023.

Silaha haramu zitapaswa kusalimishwa katika Kituo chochote cha Polisi nchini, Ofisi ya Serikali za Mitaa au kwa Mtendaji Katal Shehia kuanzia muda wa saa mbili asubuhi hadi saa kumi jioni.

Jeshi la Polisi nchini linasisitiza kuwa Mtu yeyote atakayesalimisha silaha haramu nje ya muda ulioainishwa katika tangazo la msamaha atachukuliwa hatua za kisheria. Hivyo ili kuepukana na usumbufu au kukamatwa zingatia muda wa msahama uliotolewa.

Mtakumbuka mwaka jana mwezi Septemba, 2022 Serikali ilitoa msamaha wa kutoshitakiwa kama huu, ikiwataka wale wote waliokuwa wanamiliki silaha kinyume na sheria kuzisalimisha kwa hiari, hata hivyo baadhi hawakuitikia wito huo.

Kutokana na hilo Jeshi la Polisi lilifanya operesheni mbalimbali na kufanikiwa kuwakamata na kuwafikisha mahakamani jumla watuhumiwa 221 kwa kosa la kumiliki silaha kinyume cha sheria pamoja na watuhumiwa 17 kwa kosa la kumiliki risasi kinyume cha sheria.

Jeshi la Polisi nchini, linatoa wito kwa wananchi wote wanaomiliki silaha kinyume na sheria, kuhakikisha kuwa wanatumia fursa hii adhimu ili kuepuka kukumbwa na mkono wa sheria kwa kuwa mara baada ya kipindi cha msamaha kuisha, litaendesha operesheni na msako nchi nzima ili kuwabaini na kuwakamata wale wote watakaopatikana wakimiliki silaha na risasi kinyume cha sheria.

Vilevile, tunawasisitiza wananchi wote ambao ndugu zao walikuwa wanamiliki silaha kihalali na sasa wamefariki kuhakikisha wanazisalimisha silaha hizo kulingana na masharti yaliyotajwa.

Pia, wamiliki wote wa silaha mnasisitizwa kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya matumizi mabaya na utunzaji wa silaha usiozingatia sheria na kanuni. Atakakaye kiuka sheria na kanuni husika hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake ikiwa ni pamoja kufutiwa Leseni na kufikishwa mahakamani.

Imetolewa na: David A. Misime- SACP Msemaji wa Jeshi la Polisi Makao Makuu ya Polisi Dodoma, Tanzania.
www.polisi.go.tz
www.twiter.com/tanpol www.facebook,com PolisiTanzania